Tuesday, July 30, 2013

JK ahitimisha ziara Kagera

Rais Jakaya Kikwete akihutubia wananchi kabla ya kuhitimisha ziara yake Mkoani Kagera:

Rais Jakaya Kikwete amehitimisha ziara yake Mkoani Kagera akiwatahadharisha Watanzania kuwa macho na baadhi ya watu na viongozi wa dini wanaopita huku na kule wakichochea vurugu, na kuwataka watanzania kuendelea kuienzi amani waliyonayo .

Katika siku ya mwisho ya ziara yake Mkoani Kagera , Rais Jakaya Kikwete alikutana na viongozi wa kada mbalimbali, ikulu ndogo mjini Bukoba.

Hapo Rais Kikwete pamoja na kuzungumzia jinsi serikali yake inavyotekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile umeme, maji, miundombinu, pamoja na uchukuzi, pia amewahusia watanzania kuitunza amani waliyonayo na kuwapuuza wale wote wanaotaka kuivuruga nchi kwa misingi ya dini.

Aidha Rais pia amegusia suala la ulinzi na Usalama na tatizo la wahamiaji haramu ambalo limejikita katika mikoa ya mipakani huku akiinyooshea kidole idara ya Uhamiaji.

Kabla ya kufanya majumuisho hayo, Rais Kikwete amehutubia maelfu ya wakazi wa Manispaa ya Bukoba katika uwanja wa Kaitaba ambapo Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe ametolea majibu kero ya usafiri wa majini, ilhali Mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Hamis Kagasheki akazungumzia baadhi ya kero za jimbo lake.

Kisha mgogoro wa Mradi wa ujenzi wa soko ulioligawa baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba Vipande viwili, kupatiwa suluhu na Rais Kikwete.

Rais Kikwete amehitimisha ziara yake Mkoani Kagera kwa kuzindua na kuweka mawe ya Msingi katika miradi tisa ya Maendeleo Katika wilaya za Muleba, Biharamulo, Ngara, Karagwe, Kyerwa pamoja na Manispaa ya Bukoba.

TBC

0 comments:

Post a Comment