Saturday, July 27, 2013

Rais Kikwete asema muda si mrefu malaria itakuwa historia Tanzania


Rais Jakaya Kikwete amesema serikali itaendelea kujenga zahanati kwa kila kijiji na kuimarisha vituo vya afya na hospitali ili Kukabiliana na magonjwa makubwa yanayosabisha vifo vya watu wengi ikiwemo malaria ambapo amesema muda si mrefu Tanzania itaitangazia dunia kwamba malaria Tanzania hakuna.

Akiongea kwenye mkutano wa hadhara wilayani Muleba Mkoani Kagera baada ya kuzindua mradi mkubwa wa maji utakaowahudumia wananchi wa mji wa Muleba na vitongoji vyake, rais Kikwete amesema katika juhudi hizo serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kila mwaka kwa ajili ya kutekeleza mipango mbalimbali ya afya na huduma za jamii ikiwemo huduma ya maji lakini tatizo ni baadhi ya watendaji wa Halmashauri za Wilaya ambao wamekuwa wakijihusisha na ubadhirifu wa fedha hizo

Mapema katika taarifa yake kwa Rais, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Oliver Vavunge ameeleza kuwa mradi huo mkubwa wa maji uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.3 umetekelezwa na serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa(UN-HABITAT) kupitia kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo wakati huo Profesa Anna Tibaijuka ambapo waziri wa maji Prof Jumanne Maghembe amesema serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kusambaza maji hayo kwa wananchi wa Muleba. Katika mkutano huo baadhi ya mawaziri waliofuatana na rais Kikwete ziara ya Mkoa wa Kagera wamezungumzia mipango mbalimbali na utekelezaji wa ahadi za serikali ikiwemo miradi ya ujenzi wa barabara zikiwemo za Miji Mikuu ya Wilaya na Manispaa na huduma ya usafiri wa meli katika ziwa victoria.

0 comments:

Post a Comment