Wazee waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia wameilalamikia Serikali
wakisema haionyeshi kuwajali licha ya kutoa mchango mkubwa kwa taifa.
Wakizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ambayo kimkoa
yaliadhimishwa katika Viwanja wa Naliendele na kuhudhuriwa na Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, wazee hao walidai
kwamba Serikali imekuwa ikipokea misaada kwa ajili yao lakini imekuwa
haiwafikii.
Mmoja wa wazee hao, Vicent Mshamu (91), alisema Serikali haiwasaidii
kitu chochote licha ya wahisani kutoa fedha za kuwasaidia kutokana na
mchango walioutoa kwa taifa.
“Kuna fungu linatolewa na wahisani kwa ajili ya kutusadia lakini cha
ajabu fungu hilo halitufikii sisi walengwa na hatujui jinsi gani fungu
hilo la fedha linavyotumika ukizingatia kwa sasa hatuna nguvu wala
mshahara. Ombi letu kwa Serikali ni kwamba iangalie namna ya kutusaidia
na kutuenzi watu tulioshiriki katika vita,” alisema Mzee Mshamu.
Mshereheshaji wa maadhimisho hayo, Luteni Bariki Julius Mwakivega
alisema Tanzania ilishiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa
Msumbiji kuanzia mwaka 1970.
Alisema kuwa Jeshi hilo lilishiriki katika operesheni mbili, Tegema
iliyofanyika katika Jimbo la Tetegaza na Manica na operesheni Safisha
katika Jimbo la Zambezia.
Alisema wapiganaji 101 walioshiriki katika harakati za ukombozi wa
Msumbiji walipoteza maisha na kuzikwa nchini humo kabla ya mwaka 2004.
Serikali ya Tanzania na ile ya Msumbiji ziliamua kurejesha miili ya
mashujaa hao katika ardhi ya nchi yao na kuzikwa katika eneo la jeshi la
Naliendele.
Source : mwananchi
0 comments:
Post a Comment