Showing posts with label Kitaifa. Show all posts
Showing posts with label Kitaifa. Show all posts

Wednesday, July 2, 2014

Wakazi wa Manyoni waiomba serikali kuwatatulia tatizo la maji.


Wakazi wa vijiji vya MAKALE, MITUNDU, MGANDU na ITIGI wilayani MANYONI mkoa wa SINGIDA wameiomba serikali kufanya juhudi za ziada kuwatatulia tatizo la maji katika maeneo yao.

Wakazi hao wamesema tatizo la maji limedumu kwa zaidi ya miaka 30 hali ambayo huwalazimu kukesha usiku kucha wakitafuta maji.

Wakazi hao wametoa kilio hicho mbele ya Naibu Waziri wa Maji AMOS MAKALA aliyetembelea vijiji mbali mbali wilayani Manyoni ili kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya maji.

Akijibu malamiko ya wananchi hao MAKALA amesema serikali inashughulikia tatizo la maji na hadi mwaka huu utakapokamilika tatizo hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi.


NGORONGORO: Migogoro ya wafugaji kutatuliwa.



Waziri wa Maliasili na Utalii, LAZARO NYALANDU ameagiza bodi ya Mamlaka ya NGORONGORO kutatua migogoro ya wafugaji wanaoishi katika bonde la hifadhi ya NGORONGORO kufuatia wafugaji hao kufunga bara bara kwa madai ya kupinga kujengwa kwa hoteli ya kitalii katika hifadhi hiyo bila kushirikishwa.

Akizungumza na wafugaji hao Waziri NYALANDU amesema serikali haitaruhusu ujenzi wowote ufanyike katika eneo hilo kwa sasa mpaka hapo tathmini itakapofanywa na ofisi ya makamu wa Rais mazingira na kubaini iwapo ujenzi huo ufanyike au la.

Waziri Nyalandu ambaye alikwenda NGORONGORO kuzindua bodi mpya ya hifadhi ya NGORONGORO amesema ni vema bodi hiyo ikatafuta mbinu za kutatua migogoro katika sehemu ya hifadhi.

Kuhusu suala la uwakilishi zaidi wa wafugaji katika bodi ya NGORONGORO amesema ndani ya siku SABA atateuwa mwakilishi mwingine toka katika jamii hiyo ili aweze kuingia katika bodi hiyo na hivyo kufanya idadi ya wawakilishi WAWILI.

Friday, August 9, 2013

YAMEBAKI MASAA 24 TU KWA WAHAMIAJI HARAMU KUONDOKA NCHINI KWA HIARI YAO ....WANYARWANDA 520 WAMEKWISHAONDOKA KWA HIARI


Zikiwa zimesalia saa 24 kabla ya kumalizika kwa muda uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa wahamiaji haramu kuondoka nchini au kuhalalisha ukaazi wao na wenye silaha kuzisalimisha, makundi ya wahamiaji hao, yameanza kuondoka kwa hiari.

Wastani wa wahamiaji haramu 150 wanaendelea kujiandikisha kuvuka mpaka katika Kituo cha Rusumo, Ngara mkoani Kagera kutekeleza agizo hilo.

Ofisa Uhamiaji wa Kituo cha Rusumo, Samweli Mahirane alisema mpaka sasa Wanyarwanda 520 wameshaondoka katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Ngara na kurejea makwao huku Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe akisema silaha 17 za aina mbalimbali zimesalimishwa.

Mahirane alisema wahamiaji hao wanatokea katika vijiji vya Wilaya za Ngara, Karagwe, Kyerwa, Biharamulo na Geita pamoja na Runzewe na wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo bila vibali halali.

“Kuondoka kwa hiari kwa wahamiaji haramu, kutahitimishwa Jumatatu Agosti 12 na baada ya tarehe hiyo, vyombo vya dola vitaanza kufanya kazi kama agizo la Rais Kikwete lilivyoelekeza katika Mikoa ya Kagera na Kigoma,” alisema.

Aliwahakikishia wahamiaji hao usalama katika mataifa yao kwani hivi karibuni Serikali ya Rwanda ilikubali kuwapokea hata walio na mifugo kwa masharti kuwa ndani ya kipindi kifupi wataipunguza kwa kuiuza na kuboresha maisha yao.

“Rwanda wanahitaji mifugo michache, hivyo walio na mingi wanatakiwa kuipunguza kwa kuuza na kujenga makazi bora ikiwa ni pamoja na kuhifadhi ama kulinda mazingira ya nchi hiyo,” alisema Mahirane.

Monday, August 5, 2013

MSIMAMO WA RAIS KIKWETE KWA RAIS KAGAME WA RWANDA WAUNGWA MKONO KWA ASILIMIA 100 NA WASOMI HAPA NCHINI....


WASOMI na baadhi ya wanasiasa wazalendo nchini wameunga mkono msimamo wa Tanzania uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na chokochoko zinazoanzishwa na Rwanda na wamemtaka Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame, kukaa meza ya mazungumzo na waasi wa nchi hiyo walioko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwani amani haiwezi kutafutwa kwa njia ya mtutu wa bunduki.

Akizungumza na MAJIRA kwa njia ya simu jana Mhadhiri wa Chuo cha St. Agustino, katika kitivo cha sayansi ya siasa, Prof. Mwesiga Baregu, alisema ushauri alioutoa Rais Kikwete kwa Rais Kagame ni mzuri, hauwezi kuleta athari zozote tofauti na kutumia mtutu wa bunduki kukabili waasi.

"Mimi nikiwa kama mtaalam wa kutatua migogoro suala la mazungumzo ni njia moja ambayo huwa inatumika mara kwa mara na inasaidia kuleta amani," alisema na kuongeza;

"Kutumia mtutu wa bunduki haileti tija kwa mataifa yote mawawili, hivyo ni busara itumike njia ya mazungumzo."

Alitoa mwito kwa nchi jirani kushirikiana kutatua mgogoro uliopo kwa njia ya mazungumzo baina ya Rwanda na DRC.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo cha Elimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Kitila Mkumbo, alisema anakubaliana na kauli ya Rais Kikwete na anashangazwa na Rais Kagame ni kwa nini anachukizwa kuambiwa azungumze na waasi.

"Maana yake inaonekana hataki kushauriwa...ushauri huo ni kitu kizuri kinaweza kuleta maelewano," alisema Dkt. Mkumbo. Alisema Rais Kagame, anaonekana kama dikteta kutokana na kukataa kuambiwa ukweli na viongozi wenzake.

Alisema kauli ya Rais Kikwete, aliyoitoa kwenye hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa saba hakugusia masuala ya vita na anaamini kwamba kwa karne hii sio mwafaka nchi kuingia kwenye vita kwani nchi zina matatizo mengi ambayo yanahitajika kupatiwa ufumbuzi.

"Alichoongea Rais Kikwete, ni msimamo unaotakiwa kuungwa mkono na Watanzania kwani yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu na hiyo ndiyo kauli ya nchi...hivyo alichosema ni sawa," alisema Dkt. Mkumbo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alisema ameridhishwa na kauli ya Rais Kikwete, kwani ametumia lugha sahihi katika kueleza hali halisi, hivyo Watanzania wote wanatakiwa kumuunga mkono.

Alisema kwa hali ilivyo ni lazima Watanzania waungane katika masuala kama hayo ili kuleta mshikamano wa nchi.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustino Mrema, alisema anamuunga mkono Rais Kikwete, kwa kauli yake hiyo.

Alisema Rais Kagame ameanza chokochoko dhidi ya Tanzania na kwamba hivyo, ndivyo alivyoanza hata Idd Amin. "Siungi mkono vita vitokee, lakini kama atatuchokoza basi tuwe wa mwisho kujibu mapigo," alisema Mrema.

Aliyekuwa Mhadhiri UDSM, Dkt. Azaveri Lweitama, amezitaka nchi za Afrika Mashariki kukaa chini ili kuangalia jinsi ya kutatua mgogoro huo.

Alisema kuipiga Rwanda ni kazi ndogo sana, lakini hauwezi kumaliza tatizo kwa kutumia bunduki na badala yake ni vyema nchi hizo zikaangalia namna ya kumaliza mgogoro.

"Unajua mnaweza kuingia katika vita mkamuondoa Rias wa Rwanda, lakini bado mkatengeneza matatizo mengine kwa rais ajaye," alisema.

Alisema Kongo kuna waasi wa Rwanda na hata Rwanda pia kuna waasi wa kutoka Kongo, hivyo ni lazima kutafuta njia nzuri ya kutatua tatizo hilo.

Kwa upande mwingine, Dkt. Lweitama, alivitaka vyombo vya habari kutopotosha taarifa zinazozungumzia vita vikitokea hakuna mtu atakayebaki salama.

"Vyombo vya habari vijitahidi kuandika habari zisizo za uchochoezi, kwani hata ninyi pia ni Watanzania, naamini vita ikitokea hakuna mhariri wala mwandishi atakayebaki salama," alisema.

Alisema vyombo vya habari pia vina nafasi ya kukaa chini na kutafakari namna ya kumaliza mgogoro kwa kuwa vina nafasi kubwa kwa mustakabali wa taifa.

Uhusiano wa Tanzania na Rwanda unaelekea kupata mtikisiko baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao.

Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa nia njema kwa kuwa bado anaamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike.

Ushauri ule aliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. ambapo katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli hiyo.

Tangu atoe ushauri huo viongozi wa Rwanga wamekuwa wakitoa kauli za kejeli dhidi ya Tanzania na Rais Jakaya Kikwete. Katika hotuba yake Rais Kikwete, alisema uhusiano wa Tanzania na Rwanda unapitia katika kipindi kigumu

-MAJIRA.

Sunday, August 4, 2013

UCHOCHORO WA KUVUSHA MADAWA YA KULEVYA DAR HUU HAPA


Ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Matajiri wauteka, waharibu mfumo wa ukaguzi

MFUMO wa ukaguzi wa wasafiri na mizigo yao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) umetekwa na sasa uko mikononi mwa matajiri na wanasiasa wanaofanya biashara ya dawa za kulevya hapa nchini, MTANZANIA Jumapili linaandika kwa uhakika.

Vyanzo vya habari vya kuaminika vilivyo ndani ya serikali vinavyofanya kazi bega kwa bega na dawati la habari za siasa na uchunguzi la MTANZANIA Jumapili vimedokeza kuwa, baadhi ya watoto wa viongozi wakuu wa nchi, wafanyabiashara wenye ukwasi wa kutisha na wanasiasa wenye utajiri ambao umekuwa ukitiliwa shaka kwa muda mrefu, wamebainika kuingilia mfumo wa kiitelejensia wa JNIA kwa kuupandikizia watu ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa maelekezo yao.

Ripoti ya uchunguzi wa kikachero iliyo mikononi mwa maofisa wa juu serikalini na ambayo waliinukuu katika mazunguzo yao na gazeti hili, inaeleza kuwa mtandao wa matajiri wauza dawa za kulevya umewaondoa wafanyakazi kadhaa watiifu waliokuwa katika kitengo cha ukaguzi wa abiria na mizigo cha JNIA na kupachika watu wao walio kwenye mfumo wa malipo wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Sambamba na hilo, walieleza kuwa kitengo cha kupambana na biashara ya dawa za kulevya nchini kimedhoofishwa na hata mbwa wa polisi waliokuwa wakitumika kukagua mizigo ya wasafiri wanaotumia uwanja wa JNIA wameondolewa katika mfumo wa ukaguzi na sasa watumika kwa nadra, hasa zinapovujishwa taarifa za usafirishaji wa dawa za kulevya ambazo hutolewa aghalabu wafanyabiashara hao wanapohitilafiana kibiashara na kuamua kuumbuana.

Taarifa hizi zimethibitishwa na kauli ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP) Godfrey Nzowa, ambaye katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumapili, alieleza kuwa mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya hapa nchini una pesa nyingi zinazouwezesha kufanya jambo lolote ili kufanikisha biashara hiyo.

Kamishina Nzowa, ambaye alitakiwa na gazeti hili kutoa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na matukio hayo ya dawa za kulevya, likiwemo lile la Watanzania wawili waliokamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya pamoja na uwezo wa kitengo chake wa kupambana na wauza dawa za kulevya, alisema kazi hiyo ina changamoto kubwa katika kufanikiwa kwake, kwa sababu inawahusisha watu wenye fedha nyingi hapa nchini.

Alisema, Watanzania wawili, Agnes Gerald (25) na Melisa Edward (24), waliokamatwa na kilo 150 za dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini, Julai 5, mwaka huu, walifanikiwa kupita JNIA bila kugundulika kutokana na watu waliokuwa kwenye mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo.

“Hawa Watanzania waliopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere na kukamatwa Afrika Kusini, waliweza kupita kwa sababu inategemea na watu waliokuwepo kwenye mashine za ukaguzi siku hiyo. Unajua hakuna ushirikiano wa karibu baina ya watendaji wanaohusika na udhibiti wa dawa za kulevya. Hilo ni tatizo kubwa linalosababisha vikwazo katika kupambana na mtandao wa dawa hizo.

“Sisi tunategemea kupata taarifa za wauza dawa za kulevya kutoka kwa watu, wakiwemo wakaguzi wa mizigo na abiria, hapo ndipo tunakwenda kumpekua mtu anayeshukiwa kubeba dawa hizo. Tunapopewa taarifa tunafanya ukaguzi, mbwa tunawanusisha, lakini mara chache kwa sababu wakati mwingine wanashindwa kugundua mizigo yenye dawa hizo iliyopuliziwa manukato au kunyunyiziwa kahawa,” alisema Nzowa.

Kamishina Nzowa pia alilalamika kukithiri kwa rushwa kwa watendaji ndani ya kikosi cha kupambana na dawa za kulevya pamoja na jamii kuwa ni jambo ambalo linasababisha kushamiri kwa biashara hiyo.

Mbinu mpya za kusifirisha dawa za kulevya

Duru za uchunguzi za MTANZANIA Jumapili, zimebaini kuwepo kwa mbinu mpya inayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha mizigo yao tofauti na ile iliyozoeleka.

Wafanyabiashara, wanasiasa na watoto wa viongozi wa serikali wanaojihusisha na biashara hiyo sasa wameligeukia kundi la wasanii wa filamu na wanamuziki wa kizazi kipya wanaotajwa kuwa na tamaa ya utajiri wa haraka haraka na kulifanya wasafirishaji wakuu wa dawa hizo.

Uchunguzi unaonyesha kuwa, wasanii hususan vijana, ndio wanaotumiwa zaidi kubeba dawa za kulevya huku wakihakikishiwa usalama wao na matajiri na wanasiasa wanaotajwa kuwa karibu na baadhi ya viongozi wa serikali wanaowatumia kama kinga yao, kwa makubaliano ya kugawana kipato kinachotokana na biashara hiyo au kuwa katika orodha ya malipo maalumu.

Mbinu zinazotajwa kutumika kusafirisha dawa za kulevya ni pamoja na mzigo baada ya kufungwa hunyunyiziwa pilipili, manukato au kahawa ambazo huondoa uwezo wa mbwa wenye mafunzo maalumu ya kutambua dawa za kulevya kubaini.

Imebainika kuwa dawa za kulevya zilizofungwa vizuri na kunyunyiziwa unga wa pilipili au kahawa juu yake huondoa uwezo wa mbwa kunusa harufu kwa usahihi na badala yake humfanya apige chafya.

Njia nyingine inayotajwa ni kufunga dawa za kulevya ndani ya karatasi ya kaboni ambayo mashine za ukaguzi zilizo katika uwanja wa ndege hazina uwezo wa kubaini kilichofungwa ndani pamoja na uvaaji wa nguo maalumu za ndani za wanawake zinazofahamika zaidi kwa jina la ‘tight’ zilizoshonewa dawa za kulevya ndani ambazo hazitambuliwi kirahisi na maofisa wa ukaguzi, bali humuonyesha mwanamke akiwa amejazi

TAA wagwaya

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mhandisi Suleiman S. Suleiman, alipoulizwa na MTANZANIA Jumapili namna mamlaka yake inavyokabiliana na tishio la ongezeko la upitishaji dawa za kulevya JNIA, alikataa kuzungumza lolote kwa kile alichoeleza kuwa kufanya hivyo ni kuathiri mwenendo wa uchunguzi unaoendelea.

RAIS KIKWETE AWAPA WANYARWANDA SIKU 14 ZA KUONDOKA TANZANIA.....MAMIA WAANZA KUREJEA RWANDA


Mamia ya wahamiaji haramu kutoka nchini Rwanda wakiwa na ng’ombe zaidi 900 wameanza kuondoka nchini kurejea kwao kutokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete kuwataka waondoke Tanzania kabla ya siku 14.

Aidha, imeelezwa kuwa kumekuwapo ongezeko la askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mkoani Kagera hasa wilayani Ngara hali inayozua hofu kwa baadhi ya wananchi, huku ikiongeza msukumo kwa wahamiaji haramu kuondoka.

Akiwa katika ziara mkoani Kagera, Rais Kikwete alitoa agizo la kuwataka wote waliokuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria waondoke mapema jambo lililotakiwa kuanza kutekelezwa Julai 29 na kukamilika Agosti 10 mwaka huu.

Alisema kuwa wahamiaji haramu na wale wanaoendesha ama kuhusika na ujambazi, uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua mwafaka za kuondoka mapema kabla vyombo vya ulinzi na usalama kuanza operesheni maalumu ya kuwasaka.

Tayari idadi kubwa ya wafugaji wenye makundi ya ng’ombe imeanza kuondoka kuelekea eneo la mpakani la Rusumo kutoka ardhi ya Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa agizo hilo la Rais Kikwete.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu alisema kwamba idadi kubwa ya wafugaji waliokuwa wakiishi kinyume cha sheria, imeitikia wito wa agizo la Rais na kuanza kuondoka kwa hiyari yao.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na idadi kubwa ya wahamiaji kuanza kuondoka, bado wapo ambao hawajaondoka kutokana na kudai kuwa na vibali walivyovipata kutoka Ofisi ya Uhamiaji na kubainisha kwamba vibali hivyo vitakaguliwa kwa umakini wakati wa operesheni maalumu ili kujua uhalali wake.

“Jambo hili la wahamiaji haramu lilikuwa kero kubwa, siyo tu kwa Wilaya ya Ngara, bali mkoa mzima wa Kagera, lakini tunashukuru sasa wameanza kuondoka, wamebaki hao wenye vibali. Ni lazima vibali hivyo tutavikagua maana vipo vilivyotolewa kinamna,” alieleza Kanyasu.

Alionya kwamba jukumu la kuwaondoa kwa nguvu wahamiaji haramu pamoja na wafugaji linasubiri muda wa mwisho ili kuanza kutekelezwa kama Rais Kikwete alivyoagiza.

Hofu ya Wanajeshi kuongezeka

Akizungumzia suala la wanajeshi kudaiwa kuongezeka wilayani Ngara, Kanyasu alisema kwamba katika wilaya yake kuna kikosi cha dharura kinachokaa katika moja ya kambi za JWTZ kikikuwa na idadi kubwa ya askari lakini wananchi hawakuwa na taarifa nacho ila kutokana na sababu za kiusalama.

“Unajua kuna kelele za hapa na pale na haya majibizano yanayotokea baina ya Rwanda na Tanzania. Haya ni kama yamewastua watu na kudhani kuwa askari wetu wa Kikosi cha Dharura waliopo hapa Ngara wameletwa maalumu kutokana na tahadhari,” alisema na kufafanua kuwa askari hao wapo siku zote kwa ajili ya kulinda mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kutulia na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.

Rais Kikwete aliagiza operesheni hiyo ya kuwaondoa wahamiaji haramu ifanyike katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja ikisimamiwa na vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Uhamiaji akiwaonya wahalifu kuwa hapatakuwa na mahali pa kukimbilia wala kujificha.

"TUMECHOKA KUONGOZWA NA MAKAFIRI, LIPIZENI KISASI NA MTAPATA UHAI MZURI"....HUU NI UCHOCHEZI WA SHEIKH PONDA


SERIKALI imenasa kanda za video zinazomuonyesha Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, akitoa mahubiri yanayowahamasisha waumini wa dini ya Kiislamu kuanzisha uasi dhidi ya serikali.

Tukio la kunaswa kwa kanda hizo limekuja ikiwa ni siku chache baada ya Jeshi la Polisi Zanzibar kutangaza kumsaka Sheikh Ponda kwa tuhuma za uchochezi, akingali anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Dar es Salaam kumkuta na hatia ya kosa la uchochezi.

Katika kanda hizo ambazo MTANZANIA Jumapili imefanikiwa kuziona, Sheikh Ponda, amerekodiwa akiwa katika Msikiti wa Mbuyuni, Zanzibar, alikohudhuria Mhadhara wa Dini ya Kiislamu,akiwataka waumini wa dini hiyo kuchukua hatua za kuikomboa Zanzibar kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kutoka kwenye mikono ya utawala wa makafiri.

Huku akiitikiwa kwa neno Takbir kutoka washiriki wa mhadhara huo, Sheikh Ponda anasikika akisema Zanzibar ni nchi ya Kiislamu, hivyo Waislamu wana wajibu kwa kuikomboa kutoka mikononi mwa vibaraka wanaoiongoza, aliodai kuwa wananyonya uchumi wake na kuutoroshea nje ya visiwa hivyo.

Moja ya kanda hizo iliyorekodiwa kwa muda wa saa moja na dakika ishirini na nne, ambayo Sheikh Ponda alitumia muda mwingi kusisitiza umuhimu wa Waislamu kuikomboa Zanzibar kutoka mikononi mwa aliowaita makafiri, anasikika akisema:

“Mna wajibu wa kuikomboa Zanzibar na si mnaweka vibaraka, wanateuliwa huko halafu wanakuja hapa kuwaongozeni, fedha zote zinachukuliwa hapa na kupelekwa kule kwa sababu tumepoteza nchi, tumepoteza hadhi.

“Makafiri wanatakiwa kuyaheshimu mambo matakatifu ya Kiislamu na kuyajua, kama hawataheshimu Mwenyezi Mungu alisema lazima mlipize kisasi katika mambo matakatifu. Mungu alisema ni lazima mlipize kisasi mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Mambo matakatifu yamewekewa kisasi.

“Miongoni mwa mambo matakatifu yaliyowekewa kisasi ni haki na uadilifu pamoja na dini ya Kiislamu,unapozungumzia dini ni pamoja na masheikh, hawa ni watu watakatifu, watu wenye hadhi, ni watu wakubwa na watakatifu kuliko baba mtakatifu kama wanavyosema wao.”

Sheikh Ponda pia anasikika akieleza kuwa Waislamu wamedhalilishwa kwa muda mrefu, hivyo wana wajibu wa kuikomboa Zanzibar kwa kuwa hata Mtume Mohammad aliongoza jeshi akakomboa nchi ya Maka kipindi cha Mwezi Ramadhani.

Alieleza kushangazwa na uteuzi wa Rais wa Zanzibar kufanyikia Dodoma na hata uamuzi wa kumuondoa madarakani kuchukulia mkoani humo na kutoa mwito wa jambo hilo kusitishwa.

Katika hili anasikika akisisitiza kuwa; “Hakuna mtu ambaye haelewi kwamba Zanzibar ipo mikononi mwa watu wasio stahiki, Zanzibar ni nchi ya Waislamu. Sisi Waislamu wa Zanzibar tuna mazingatio makubwa kuliko watu wengine kipindi hiki cha Mwezi Ramadhani kwa sababu mafundisho tunayoyapata katika maisha ya Mtume Mohammad ni sawa na mazingira ya sasa, hivyo tunatakiwa kuyatekeleza. Zanzibar si nchi ya watu, bali ni ya Waislamu.

Katika mahuburi yake kwenye mhadhara huo, Sheikh Ponda anakisika akieleza kuwa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umezaa ufisadi visiwani humo na kurejea kauli aliyodai kutolewa na Mtume iliyokuwa ikiwaonya Wazanzibari kutoruhusu uwepo wa Muungano.

“Tangu lini bia, ukahaba ukawa hitajio la Wazanzibari na hii ndiyo ‘product’ iliyotokana na Muungano na Mapinduzi.Maovu ambayo hamkuyapata kuyaona ni kauli ya Mtume, alisema mkiruhusu muungano ufisadi unatokea. Leo hii mnaona nchi ya Zanzibar mambo ambayo si hitajio la Wazanzibari, mmeingiza watawala waovu katika ardhi hii.

“Zanzibar ina watu wenye akili kubwa, wenye uwezo na ina wasomi wa fani zote na ni watu wa kuigwa duniani kote…. hivi sasa Mwislamu anapokwenda mahakamani anayesikiliza shauri ni kafiri. Mwislamu anapofunguliwa kesi, sheria hazifuatwi kwa maana kwamba kuna utaratibu wa dhamana, lakini hautolewi, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwakandamiza Waislamu.

“Leo hii viongozi wetu wanatiwa jela bila sababu, kosa lao ni pale wanapotetea Uislamu. Wako gerezani, tutapataje sifa ya Ramadhani tusipowatoa hawa ndugu zetu walioko gerezani na Mungu anasema mambo matakatifu yanalipiziwa kisasi.

“Kila siku viongozi wa Kiislamu wanauawa, Sheikh Hamis ameuawa anatoka msikitini, kafa na hakuna maelezo kwa sababu kwa mujibu wa sheria, lazima kuwe na maelekezo na mahakama iseme. Yote hayo hakuna maelezo yoyote utadhani kafa paka, kapigwa risasi kafa hakuna maelezo yoyote ya serikali.

“Ndugu zangu hali ni mbaya sana, watu wanapanga mikakati kwa ajili yenu ninyi. Msifikirie kuwa jamii haiwezi kutoweka.

'Tujenga utayari kwa ajili ya kupigania dini ya Mwenyezi Mungu, hilo ni jambo la msingi. Ukimya wenu ni tatizo kubwa sana, hivi ndivyo wanavyotaka wafike mahala wakamate mashekh wawaweke ndani, halafu mkae kimya, hili jambo ni kubwa na ni la dini, mnatakiwa msimame kidete kwa ajili ya jambo hili.

“Suala la kisasi lina uhusiano na uhai, mtapata uhai mzuri katika kulipiza kisasi ninyi Waislamu.”

Akizungumzia kukamatwa kwake hapo awali, alisema ulikuwa ni mkakati uliopangwa Dodoma, baada ya kusikilizwa kwa malalamiko ya waumini wa dini ya Kikristo.

Mbali na hayo, kauli nyingine zinazoelezwa na baadhi ya watu walioona na kusikiliza kanda hizo kuwa zina kila dalili ya kuhatarisha amani nchini, ni ile anayosikika akisema; “Sisi viongozi ndio tunatoa maagizo tuingie barabarani hata kama serikali imepiga marufuku. Kama wataleta jeshi sisi tunakuwa ‘front.’

“Kama wewe unaogopa polisi itakapofika Jihad utatoka, hawa ni watu kama wewe, anavyokupiga kirungu hakuna sababu ya kumwogopa binadamu mwenzako, hizo ni hatua za kujenga nafsi na utayari.

“Kipindi cha uchaguzi mkitumie vizuri, muwatoe hawa madarakani, watoeni wakatae halafu kimbembe kianze pale, mnatoa kauli ya moja kwa moja. Waambieni kuwa ninyi na sisi ni moto na baruti.

“Kwa upande wa Katiba, kuna suala la kupiga kura, hakikisheni kura yenu izingatie maslahi yenu. Kule Bara tulipendekeza mahakama ya kadhi imetupwa na sasa hivi kazi zile ambazo zinatakiwa kufanywa na mahakama ya kadhi zinafanywa na mahakama ya mwanzo.”

Wanafunzi 5,000 washindwa kujiunga vyuo vikuu

Pazia la udahili huo kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu, lilifungwa rasmi Julai 5, mwaka huu. Hadi wakati unafika tarehe hiyo, wanafunzi waliokuwa wameomba nafasi hiyo ni 39,140.



 Siku chache baada ya kufungwa kwa pazia la udahili kwa wanafunzi wa kidato cha sita walioomba kujiunga na vyuo vikuu nchini, imebainika kuwa zaidi ya wanafunzi 5,000 wameshindwa kujiunga na vyuo hivyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo matumizi ya mtandao wa kuomba udahili.
Pazia la udahili huo kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu, lilifungwa rasmi Julai 5, mwaka huu. Hadi wakati unafika tarehe hiyo, wanafunzi waliokuwa wameomba nafasi hiyo ni 39,140.
Matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, yanaonyesha kuwa watahiniwa 50,611 walifanya mtihani huo na kati yao 44,366 sawa na watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,242 sawa na asilimia 93.92 ya waliofanya mtihani huo.
Watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo walikuwa ni 7,659 na waliofaulu ni 4,124 sawa na asilimia 53.87. Kutokana na matokeo hayo, watahiniwa wote waliofaulu ni 44,366, hivyo kufanya wanafunzi walioshindwa kujiunga na vyuo vikuu kuwa 5,226.
Mkurugenzi wa Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu wa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), Dk Savinus Maronga alisema, wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kuomba kujiunga na vyuo vikuu ni 39,140 na kwamba vyuo vikuu nchini vina uwezo kwa kuchukua wanafunzi 60,000.
Dk Maronga alisema hali hiyo inatokana na baadhi yao kutokuwa na sifa zinazotakiwa kuweza kuomba udahili wa kumwezesha kusoma elimu ya juu.
“Kuna baadhi hawana sifa ‘Eligibility’ za kuweza kuchaguliwa kuingia Chuo Kikuu. Hivyo ili uweze kudahiliwa kuendelea na elimu ya juu ni lazima uwe na vigezo. Kuhusu mfumo sidhani kama ulikuwa na matatizo yeyote,” alisema Dk Maronga
Kauli za Wanafunzi
Wanafunzi waliozungumza na gazeti hili kuhusu mfumo huo wa udahili wa mtandao, walisema una usumbufu kutokana na wengi kutokujua kuutumia.
Frank Mabagala aliyehitimu Shule ya Sekondari Pugu Jijini Dar es Salaam, alisema wanafunzi walio wengi wameshindwa kuutumia mfumo huo kwani una mambo mengi ya kufanya.
“Nilijaza fomu vizuri tu, lakini sikuwa najua kama kuna wakati nilitakiwa kwenda kuangalia ‘Eligibility’ hadi nilipoambiwa na rafiki yangu kwenda kuangalia ‘Eligibility’ na kukuta kuna nafasi imeandikwa ‘NO’ hapana vyuo vyote nilivyochagua,” alisema Mabagala.
Alisema hata upatikanaji wa vocha za TCU bado zilikuwa tatizo, kutokana na kupatikana sehemu moja tu ya Benki ya NBC. Hivyo kwa watu wanaoishi pembezoni mwa benki hiyo kuwawia vigumu kupata huduma hiyo kwa haraka.
“Mfano mimi ninaishi Tegeta lakini nilikwenda benki pale Tegeta nikakuta zimekwisha,.Nikaenda Mliman City nako nikakuta vivyo hivyo hadi nilipokwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ndipo nikazikuta nako kulikuwa na foleni,” alisema Mabagala na kuongeza:
“Kama Dar es Salaam upatikanaji wa vocha inakuwa hivi, je, kwa wanaoishi pembezoni mwa mkoa ambako benki kuifikia ni kazi, watu wa aina hii watakuwa wamepata usumbufu mfano ni rafiki zangu watatu wa mkoa walinitumia fedha huku ili niwanunulie vocha na kuwatumia.”
Naye Zahora Miraji aliyehitimu kidato cha sita Shule ya Seminari ya Ridwaa jijini humo, alisema alijaza fomu kulingana na maelekezo yalivyokuwa, lakini katika hali ya kushangaza amekuta kile alichokijaza kimebadilishwa.
Miraji alisema, katika chaguo la vyuo, chaguo la kwanza na pili aliomba Chuo cha Mkwawa, la tatu na nne aliomba Chuo cha Dodoma na chaguo lake la tano aliomba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini alipokwenda kuangalia kwa mara ya mwisho akakuta amebadilishiwa.
“Nilijaza vizuri na nilipokuwa nikifungua kuona kinachoendelea ninakuta bado iko katoka ‘mchakato’ lakini nilipokwenda tena kuangalia nikakuta vyuo nilivyoomba vya Mkwawa, Dodoma na Dar es Salaam vyote vimebadilishwa sasa sikujua tatizo ni nini,” alisema Miraji na kuongeza:
“Nilikuta chagua la kwanza na la pili nimeandikiwa chuo cha Jordan na hata sijui kipo wapi na chaguo la tatu hadi la tano Chuo cha Usafirishaji Marrine. Nilikwenda TCU kuwaeleza kilichotokea wakanipa fomu nikaijaza kuonyesha tatizo langu sasa sijui kama watalishughulikia au la.”
Kauli ya Chuo

CLINTON ATUA BONGO KIANA KUKAGUA MIRADI YAKE


Dar es Salaam. Rais wa Mstaafu wa Marekani, Bill Clinton jana alifanya ziara katika makazi ya watu duni eneo la Vingunguti, wilayani Ilala Dar es Salaam, ambapo alikagua miradi midogomidogo ya wananchi inayofadhiliwa na mfuko wake (Bill Clinton Foundation).

Clinton alitembelea eneo hilo akitokea moja kwa moja Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam (JNIA), alipowasili akiwa katika ziara ya nchi mbalimbali za Afrika kukagua miradi inayoendeshwa na mfuko wake.

Katika eneo hilo rais huyo mstaafu alipokewa kwa shamrashamra mbalimbali ikiwamo ngoma za kiasili huku baadhi ya wananchi wakipigwa butwaa na kutoamini macho yao kwa kiongozi huyo kutembelea makazi yao.

Aidha, Clinton alipata wasaa wa kusalimiana na wakazi wa Vingunguti wakiwamo watoto ambao walishindwa kuzuia hisia zao wakijaribu kumsogelea, hali iliyomsukuma Clinton kuwasogelea na kuwasalimia kwa kuwashika mikono.

Maneno ya ‘Welcome Vingunguti Clinton‘ yalisisika kutoka kwa wananchi kuashiria kumkaribisha rais huyo wa 42 wa Marekani wakati alipowasalimia akitumia takriban dakika 15.

Clinton alikagua miradi ya midogomodogo ya wananchi iliyo chini ya mfuko wake ikiratibiwa na kutekelezwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Plan) pamoja na Benki ya Barclays kupitia Vikoba.

Miradi aliyokagua ni pamoja na saluni za kinamama, ushonaji na chips ambapo pia alishuhudia mmoja wa wanachama wa vikundi hivyo akikabidhiwa mkopo wa Sh100,000 ambaye alieleza mbele ya Clinton kuwa atazitumia kwa mradi wa maandazi, hali iliyomfanya rais huyo na umati wa watu uliohudhuria kucheka.

Akizungumza katika ziara hiyo Clinton alizishauri benki nchini, kuwekeza kwenye vikundi vya kuweka na kukopa (Vikoba) akieleza kuwa ndiyo mkombozi kwa wananchi hasa wanawake.

“Nimekuwa kwenye miradi hii kwa miaka 30 kabla sijawa rais, hivyo basi najua umuhimu wake. Benki zinatakiwa zisaidie Vikoba kwani vikundi hivyo huwafikia wananchi kwa haraka na wepesi hivyo basi kunahitajika njia mbadala za kuhakikisha vinakuwa imara,” alisema Clinton na kuongeza;

“ Raha ya maendeleo ni kuona watu wanajitegemea wenyewe katika shughuli za kujiingizia kipato.”

Mmoja wa wananchi walionufaika, Zainab Paul ambaye ni mwanachama wa Kikundi cha Amani Hisa alisema kuwa kupitia Mfuko wa Bill Clinton na Vikoba ameweza kujikwamua kimaisha ikiwamo kumlipa mtoto wake karo ya shule.

“Kikundi chetu kina wanachama 30 na huwa tunanunua hisa kwa Sh2000 na kila mwanachama anaruhusiwa kukopa zaidi ya mara tatu,” alisema Paul.

Clinton alieleza kufurahishwa kwake na hatua walizofikia wakazi hao wa Vingunguti akiwapongeza kinamama kwa jitihada zao na baada ya ziara hiyo alielekea Ikulu kwa mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Plan, Tanzania, Jorgen Haldorsen alisema shirika lake limekuwa likihudumia nyanja za kiuchumi na kijamii kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa kada ya chini wanapata huduma mbalimbali ikiwamo afya.

Naye, Mshauri wa Mambo ya Kujikimu wa Plan Stella Tungaraza aliwataka wananchi kujiunga zaidi na Vikoba na kwamba shirika lake limepanga kuanza kutoa mafunzo ujasiriamali kwa vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Baadaye Rais Clinton alitia saini makubaliano ya taasisi yake ya Bill Clinton Foundation kusaidia sekta ya kilimo nchini.

Makubaliano hayo yalitiwa saini Ikulu jijini Dar es Salaam na Sophia Kaduma ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Chakula pamoja na mwakilishi wa taasisi ya rais huyo mstaafu, Walker Morris.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Clinton alisema wakulima wa Tanzania wanatakiwa kutambua kuwa kuna nchi nyingine zinashindwa kuendesha shughuli za kilimo kutokana na uhaba wa ardhi au kuwa na ardhi isiyokuwa na rutuba na kuwataka watumie fursa hiyo kukuza uzalishaji wa kilimo .