Showing posts with label Jamii. Show all posts
Showing posts with label Jamii. Show all posts

Thursday, July 3, 2014

Sakata la Mbasha...


Mambo juu ya mambo! mvumo mkali wenye kuogofya unaendelea kutamalaki katika ndoa ya wanamuziki zao la upako wa Injili Bongo, Emmanuel na Flora Mbasha, safari hii ‘topiki’ siyo zile tuhuma za ubakaji zilizopo mahakamani.



Mbeba ‘niuzi’ wa awamu hii ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, baada ya Mbasha kuona isiwe tabu, hivyo kuamua kupambana na mtumishi huyo wa Mungu kwa njia ya kiroho zaidi.

Mbasha baada ya kulieleza gazeti mama la hili, Uwazi lililoandika habari yenye kichwa “Mbasha: Gwajima Niachie Mke Wangu”, akiidadavua dhana yake kwamba hapendi ufadhili wa Gwajima kwa mkewe, yaani Flora sasa ameamua kwenda mbele zaidi.

Habari zinadai kuwa, mbele ya Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Mkoa wa Dar es Salaam, Bruno Mwakibolwa ambalo Gwajima ni memba hai, ameshapokea mashitaka kuhusu mchungaji huyo kuhusika kuitikisa ndoa ya waimbaji hao wa Neno la Mungu na mlalamikaji ni Mbasha mwenyewe.
Wikiendi iliyopita, Mbasha aliketi na kiongozi huyo na kushusha tuhuma zake dhidi ya Gwajima kama zilivyothibitishwa na mlalamikaji mwenyewe, nazo ni hizi zifuatazo.

MOSI; Gwajima ni kiongozi wa kiimani wa Mbasha na Flora lakini tangu matatizo ya ndoa yao yalipojitokeza, mchunga kondoo huyo wa Bwana hajawahi kufanya lolote kunusuru muunganiko huo uliohalalishwa kwa jina la aliye juu.



PILI; Gwajima anajua kila kitu kuhusu mgogoro wa Mbasha na mkewe lakini kipindi chote cha matatizo, Kanisa la Ufufuo na Uzima limekuwa mfadhili wa Flora kwa sehemu kubwa. Hapa anauliza, huu ufadhili una kipi nyuma yake?

TATU; Gwajima anatambua kuwa Flora ni mke wa mtu, mwenye mali ameshaomba aachiwe mwandani wake bila mafanikio. King’ang’anizi kina msukumo upi?

NNE; Gwajima amekuwa akimuumiza Mbasha kihisia, kiakili na kiroho kwa sababu yeye anagombana na mkewe lakini mchungaji huyo bila kufikiria maumivu aliyonayo, humwita Flora madhabahuni katika ibada na kumpa nafasi ya kuimba.

TANO; Flora anaishi hotelini na yeye mwenyewe alishakiri kuwa fedha za kulipia hoteli alizipata kutokana na michango ya waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima. Hapa Mbasha analalamika, inakuwaje kanisa limfadhili mke wa mtu kuishi hotelini ikiwa mumewe hajui?

SITA; Katika hoja zote hizo, Mbasha amelieleza Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste kuwa hana imani na Gwajima kwa vile kama ni busara baada ya kuona ndoa hiyo imetikisika yeye (Gwajima) angekaa pembeni kwa namna yoyote ile, hivyo Mbasha akaiomba menejimenti ya baraza hilo kumpa adhabu kali mwenzao.
Mbasha alipozungumza na Amani, Jumanne iliyopita, alisema baraza hilo liliahidi kushughulikia shauri lake na uamuzi utachukuliwa baada ya kumwita Gwajima na kumsikiliza kwa upande wake.

WENYE KWENU KWAHERI!
Kesi ya Mbasha kudaiwa kumbaka shemeji yake ilipoanza, mume huyo wa Flora alikimbilia mafichoni, kwa hiyo swali kwamba anaabudu kwenye kanisa gani halikuwa na mashiko kwa sababu mhusika mwenyewe hakuwa akionekana.

Baada ya Mbasha kujitokeza na kufikishwa mahakamani, kupelekwa mahabusu kwenye Gereza la Keko kabla ya kuachiwa kwa dhamana, ndipo swali kuwa anaabudu kanisa gani lilipoanza kutokana na ukweli kuwa yupo uraiani kwa ‘bondi’.


Swali hilo lilitokana na hoja kwamba kabla ya mgogoro na mkewe walikuwa wakisali kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Gwajima ambaye alishamtuhumu kumfadhili Flora na akamtaka amwachie ‘waubani’ wake huyo ili maisha yaendelee.

Mchungaji

Jawabu la swali hilo, lilijibiwa Jumapili iliyopita baada ya Mbasha kutinga Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), maarufu kama Mito ya Baraka, linaloongozwa na Mchungaji Bruno Mwakibolwa, na kukamilisha haja zake za kuabudu pale.

Mbasha alipozungumza na Amani kuhusu kusali kwa Mchungaji Mwakibolwa badala ya kwa Gwajima, alijibu: “Nimehama Kanisa la Ufufuo na Uzima, sisali tena kule. Kuanzia sasa shughuli zangu za kuabudu nitazifanyia Mito ya Baraka kwa Mchungaji Mwakibolwa.

“Siwezi kwenda kwa Gwajima kwa sababu simuelewi na ndiyo maana nimeamua kumshtaki kwa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste. Roho yangu ya kuabudu isingekuwa timilifu, ingejaa mashaka kwenda sehemu ambayo imenijeruhi na nisiyoiamini.

“Kwa kifupi si kwamba nimeanza kuabudu Mito ya Baraka hili ndilo kanisa letu tangu zamani, mimi na mke wangu. Tulihamia Kanisa la Ufufuo na Uzima baada ya Gwajima kutushawishi, kwa hiyo nimerejea kundini.
MCHUNGAJI MWAKIBOLWA
Juzi, Amani lilimsaka Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Mkoa wa Dar es Salaam, Mchungaji Mwakibolwa lakini simu yake ilipokelewa na kusikika sauti za watu wakiwa kwenye maombi kama si ibada.
GWAJIMA
Baada ya hapo, Amani lilimsaka Mchungaji Gwajima kwa njia ya simu yake ya mkononi lakini yeye hakupokea hata pale alipopigiwa kwa kurudiarudia.
KESI YA MBASHA
Kesi ya Mbasha kudaiwa kubaka itatajwa tena Julai 17, mwaka huu kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
VIPI KUHUSU KUPATANA?
Wiki iliyopita katika Gazeti la Risasi Jumamosi kuliandikwa habari yenye kichwa; MBASHA, FLORA WAPATANA. Katika habari hiyo ilidaiwa wawili hao walipatana lakini walibakiza kikao kimoja cha kumalizia taratibu zote.

Habari zinasema, taratibu hizo zinandelea licha ya Mbasha kumshitaki Gwajima kwenye Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Mkoa wa Dar es Salaam.

Source: Global Publisher

Tuesday, July 1, 2014

Mwenge wa uhuru umeendelea na mbio zake katika mkoa wa NJOMBE


Mwenge wa uhuru umeendelea na mbio zake katika mkoa wa NJOMBE kwa kukimbizwa katika wilaya ya WANGING’OMBE ambako kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka huu RACHEL KASSANDA amewataka watanzania kuwapuuza wanasiasa wanaowapotosha wananchi wasishiriki katika shughuli za Maendeleo.

KASSANDA ametoa wito huo baada ya kuzindua, kufungua na kuweka mawe ya Msingi katika Miradi TISA ya maendeleo ambayo wananchi wa WANGING’OMBE wamechangia nguvu zao katika ujenzi wake.

Amesema watanzania wasikubali kuibomoa nchi yao bali wailinde waipiganie na kuitetea dhidi ya wanaoichafua

Watu watatu wamefariki kumi wamejeruhiwa katiak ajali Singida.


Watu watatu wamekufa na wengine kumi wamejeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Noha kupasuka tairi ya nyuma na kubingirita mara tatu katika kijiji cha Januka manispaa ya Singida.

Akithibitisha kitokea kwa vifoo hivyo mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Singida daktari Deogratias Banuba amesema wamepokea maiti mbili wakiwa wamesha fariki eneo la tukio akiwemo dereva wa Noha bwana Enock Mbaga, binti Ajira Juma na maiti nyingine ya Bi Tatu Bunku ambaye alikuwa herd mistres Ngimu sekondari amefia katika hospitali ya mkoa wa Singida.
 
Daktari Banubasi amesema majeruhi kumi wamepatiwa huduma  ya kushonwa  sehemu mbalimbali za miili yao na wanaendelea na matibabu ,pia hakuna majeruhi ambaye atapatiwa rufaa . 
Mmoja wa majeruhi akiongea kwa shida huku akiwa amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Singida bwana Ramadhani Mlenga amesema gari halikuwa katika mwendo wa kasi na gafla likaacha njia na kupinduka mara tatu. 

Sunday, August 4, 2013

KAHAMA YAANZA MIKAKATI YA KUWAOKOA MAKAHABA KWA KUWAWEZESHA KIUCHUMI


Zaidi ya wanawake tisini wanaofanya biashara ya ngono wilayani Kahama mkoani Shinyanga wanatarajia kunufaika na mradi mpya wa kuwakomboa kutoka kwenye biashara hiyo, unaoratibiwa na HUHESO Foundation kwa ufadhili wa Rapid Funding Envelop (RFE).

Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi wa shirika hilo Juma Mwesigwa wakati wa utambulisho wa mradi huo kwa wadau na waandishi wa habari katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Kaltas mjini Kahama.

Mwesigwa amesema lengo la mradi huo ni kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI na kuwaondoa wanawake wanaofanya biashara ya Ngono wilayani humo. Mwesigwa amesema kuwa wanawake arobaini watapatiwa mafunzo ya cherehani na baada ya mafunzo kila mmoja atapatiwa cherehani yake mpya huku wengine hamsini wakipatiwa mafunzo ya ujasiriamali.

Awali akizinduwa rasmi mradi huo, Kaimu mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Kahama Lucas Makurumo aliwata wananchi kuupokea na wakina dada wajiunge pasipo woga kwa faida zao na Taifa kwa ujumla.

Mradi wa kuwakomboa wanawake wanaofanya biashara ya ngono wilayani Kahama utakaotekelezwa ndani ya mwaka mmoja unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 146. Mradi huo utatekelezwa katika kata Malunga, Mohongolo, Kahama Mjini, Nyihogo, Nyasubi, Nyahanga, Majengo, Mwendakulima, Kagongwa na Mungula.

Source: Mpekuzi

Saturday, August 3, 2013

Feza Kessy akata tamaa.... kura yangu na yako itambakisha Big Brother


Feza Kessy ameonesha kukataa tamaa na uwezekano wa kupona panga la kesho kwenye eviction ya Big Brother Africa.

Wakati akifua nguo zake bafuni, mrembo huyo alipewa kampani na Beverly na Elikem na kuwaambia kuwa haoni dalili kama ataukwepa msumeno wa kesho.

“Hakika, kama nitapona eviction ya Jumapili hii itakuwa ni miujiza tu,” alisema Feza.

“Ni ngumu kwa wapenzi kwenye nyumba hii. Angalia kilichotokea kwa LK4 na Koketso. Wote walitolewa usiki mmoja. Nadhani kitu kile kile kinaenda kutokea kwetu.”

Friday, August 2, 2013

Mke wa Dr. Slaa azua balaa Mahakamani


JOSEPHINE Mushumbusi, mke wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, jana alisababisha vicheko mahakamani baada ya kushindwa kumtambua mshtakiwa anayedaiwa kumpora maeneo ya SUMA JKT.

Josephine alimuacha mshtakiwa katika kesi yake na kumtambulisha mshitakiwa wa kesi nyingine kuwa ni miongoni wa watuhumiwa waliomvamia.

Hayo yalitokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa alipokuwa akitoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Leonard Chalo.

Washitakiwa katika kesi hiyo ambao wanakabiliwa na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha ni Getisi Mturi, Gake Mwita, Salum Mpanda na Charles Chasens.

Mturi na wenzake wanadaiwa Julai 13, 2011, eneo la Suma JKT makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi, walimvamia Josephine na kumpora vitu mbalimbali na kabla ya kufanya uhalifu huo walimtishia kwa silaha.

Josephine alidai Julai 13 mwaka 2011, aliingia ofisini kwake katika jengo la Mawasiliano Tower saa 2.00 asubuhi na kutoka saa 11.00 jioni kwenda nyumbani kwake eneo la Boko akiendesha gari aina ya Toyota Harrier.

Alidai akiwa eneo la tukio katika foleni alimwona mtu akipita mkono wa kushoto huku akimuangalia kwa kutumia kioo cha pembezoni na ghafla alimuona akivunja kioo cha gari lake.

Josephine aliidai alipoanza kuvunja dirisha alitahamaki lakini alisikia risasi hivyo aliamua kutafuta jinsi ya kujiokoa kwa kutoa gari eneo hilo na kwenda katika geti lililopo karibu na Suma JKT.

“Nilifanikiwa kuona sura ya mtu aliyenivamia kwa kuwa tulisimama wote kwa takribani dakika nane,”alidai Josephine.

Josephine alidai katika tukio hilo anakumbuka kulikuwa na watu si chini ya sita na walimwibia vitu mbalimbali. Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa Agosti 7 mwaka huu.

Thursday, August 1, 2013

INAUMA SANA: Kansa ya Ngozi yamharibu mtoto wa miaka 7.... Baba chozi lamtoka kuomba msaada


MTOTO Ashura Mustapha (7) mkazi wa Mwandege, wilayani Mkuranga, Pwani anasumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya ngozi tangu akiwa na mwaka mmoja.

Akizungumza na mwandishi wetu, baba mzazi wa mtoto huyo, Mustapha Makombe alisema: “Mwanangu anateseka sana jamani, ugonjwa ulianza kama malengelenge akiwa na umri wa mwaka mmoja tukawa tunakwenda hospitali ndogondogo lakini baadaye tukaamua kumpeleka Muhimbili ambapo tulipewa barua ya kutuelekeza kwenda CCBRT, kule ndipo wakagundua mwanangu ana kansa ya ngozi steji ya nne.



“Baada ya kuhangaika katika hospitali nyingi bila mafanikio, nikaamua kwenda Hospitali ya Regency (Dar) kuomba msaada wa kwenda kutibiwa India.

“Pale waliniambia nichangie shilingi milioni moja na laki tano kwa ajili ya tiketi na viza ili mwanangu akatibiwe India, hizo hela mimi sina. Naomba Watanzania mnisaidie hata kwa fedha za mitandao kwa namba 0769 517765 na 0715 424697 ili niweze kumpeleka mwanangu India akatibiwe,” alisema baba mzazi.




Mwalimu Mkuu wa Shule ya Chalinze ahamishia Ofisi chooni


MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Chalinze Mzee, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Elias Kapama, yuko katika wakati mgumu baada ya kuhamishia ofisi yake kwenye vyoo vya wanafunzi kutokana na jengo la ofisi yake kuharibika vibaya.

Hatua ya kuhamia chooni ilitokana na mkuu huyo kutawaliwa na hofu ya ubovu wa ofisi yake, hivyo kushindwa kufanya kazi zake kwa ufasaha unapotokea upepo au mvua.

Novemba 2012, Kapama alihamishia ofisi yake katika jengo la vyoo vya wanafunzi ambavyo havijaanza kutumika tangu ujenzi wake ukamilike mwaka 2011.

Akizungumzia hali hiyo, Kapama alisema kuwa anajisikia vibaya kutumia chumba maalumu cha kubadilishia nguo cha wavulana katika choo hicho kutokana na kukosa msaada kutoka halmashauri ya wilaya hiyo.

Alisema kuwa ni miezi tisa sasa tangu ahamishie ofisi yake chooni na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na ngazi ya wilaya pamoja na kufahamu mazingira hayo, hali aliyodai kuwa inamweka katika wakati mgumu.

“Sina ofisi, nimelazimika kuomba kwa wafadhili waliotujengea vyoo kwa ajili ya wanafunzi niweze kutumia chumba hiki cha kubadilishia nguo kama ofisi yangu hadi pale tutakapojenga ama kufanyia ukarabati ofisi ya zamani,” alisema.

Vyoo hivyo ambavyo vimejengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Ebenezer Spritual Center ya mjini Chalinze, vimegharimu kiasi cha sh milioni 70 hadi kukamilika.

Mkuu huyo aliongeza kuwa kwa sasa walimu wanatumia tundu moja la choo huku wanafunzi 450 wakitumia matundu saba, matatu kwa wanawake na manne kwa wavulana.

Hata hivyo mwandishi wetu alishuhudia choo hicho kinachotumika sasa kikiwa hakina hadhi na usalama kwa watumiaji.

Aliuomba uongozi wa wilaya pamoja na wizara ambao umetembelea shule hiyo na kushuhudia mazingira hayo magumu kufanyia utekelezaji wa ujenzi wa ofisi hiyo haraka ili aweze kuhama kutoka chooni.

Wednesday, July 31, 2013

NIDA yaendelea na zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa


Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) hivi sasa inaendesha zoezi la uchukuaji wa alama za vidole, kuweka saini za kielektroniki na kuwapiga picha wakazi wa jiji la Dar es Salaam ikianzia wilaya ya Temeke. Hivi sasa zoezi hili linafanyika katika Kata za Charambe, Kiburugwa, Mbagala Kuu, Taangoma na Kijichi.


Azzan: "Nipo tayari kupigwa Risasi kama ikithibitika najihusisha na Madawa ya kulevya"


Wakati Jeshi la Polisi likitoa visingizio kwamba linashindwa kunasa watuhumiwa wanaosafirisha dawa za kulevya wanaopitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kutokana na kukosekana kwa vitendea kazi, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, amesema yupo tayari kupigwa risasi au kunyongwa hadharani kama itathibitika anahusika na biashara hiyo.

Azzan alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One kuhusu kuwapo kwa madai ya barua iliyoandikwa na Mtanzania aliyefugwa Hong Kong nchini China akimtaja kuhusika na biashara ya dawa hizo.

Alisema hahusiki kwa namna yoyote ile na biashara ya dawa za kulevya au biashara yoyote haramu na kwamba taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya kijamii ni za upotoshaji na zimetolewa kwa lengo la kumchafua.

“Nimejipeleka polisi kwa mara nyingine tena na nimewaomba wafanye uchunguzi wa kina na kama nitabainika nahusika na biashara hiyo niko tayari kupigwa risasi hadharani, lakini pia sitendewi haki kwa wale ambao wanazusha jambo hili wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.

Azzan aliongeza kuwa hayupo juu ya sheria hivyo ikithibitika kuna mtu anamtuma dawa za kulevya kupitia bandari fulani pia atakuwa tayari kuwekwa hadharani na kunyongwa maana atakuwa hafai kuendelea kuwapo Tanzania.

Alisema makundi yanayomwandama ni ya kisiasa kwa lengo la kutaka kumdhoofisha katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.

Mahojiano kati ya Azzan na radio yalikuwa kama ifuatavyo;

RADIO: Mhe Idd Azzan wewe ni mbunge wa Kinondoni inaelezwa kuwa wewe ni mmoja kati ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na mmekuwa mkipokea mizigo kupitia maboti makubwa yanayotoka Pakistan yanayopitia Bagamoyo, Tanga, Mtwara na Dar es Salaam, hebu tujuze na wajuze Watanzania hili lina ukweli gani.

AZZAN: Hata mimi nimesikia hilo na bahati nzuri nimesoma kwenye mitandao kadhaa imeandika hivyo na kuna barua inayodaiwa kuandikwa na mfungwa mmoja ambaye amedai mimi ndiye nahusika kumtuma yeye.

Napenda kuwajulisha Watanzania sihusiki kwa namna yoyote ile na biashara ya dawa za kulevya na siyo dawa za kulevya tu lakini pia biashara yoyote haramu sijawahi kufanya katika maisha yangu.

Niseme tu kuwa hizo ni taarifa ambazo zimetolewa kwenye mitandao ili kuaminisha watu hivyo, lakini kimsingi sihusiki na sijihusishi na biashara ya namna hiyo.

Baada ya kuziona habari hizi kwenye mitandao nilichokifanya na sababu ilishawahi kujitokeza tena na viongozi wangu wa CCM walishawahi kuyasema hayo kwenye mkutano wa vijana nikawaambia polisi wachunguze ili kupata ukweli wa hilo jambo.

Kama itabainika nahusika basi nichukuliwe hatua za kisheria mimi siyo Mungu wala sipo juu ya sheria, nimefanya hivyo kwa maana ya kuongea na Jeshi la Polisi nimejipeleka nimetoa maelezo na nimewataka polisi kwa sababu ni kazi yao wafanye uchunguzi wa kina, pili kama nahusika na tuhuma hizo hatua za kisheria zifuatwe dhidi yangu na kama siyo kweli hao wanaoeneza uzushi huo pia wachukuliwe hatua.

RADIO: Unadhani kwa nini Mtanzania aliyeshikiliwa Hong Kong amekutaja wewe kuhusika na biashara hiyo?

AZZAN: Kwanza mimi siamini kwamba kuna Mtanzania anayeshikiliwa Hong Kong ambaye amenitaja mimi, sababu hiyo biashara kwanza sijawahi kuifanya, mimi niliiona hiyo barua haina jina la huyo Mtanzania mnayemsema, wala hakuna namba ya mfugwa sasa mfungwa anatakiwa kuwa na namba, asitaje jina ataje basi walau namba yake pia hakuna jina la gereza, kwa hiyo mimi siamini Mtanzania ambaye amefugwa kwa tuhuma za dawa za kulevya anitaje mimi kuwa nimemtuma. Hakuna hicho kitu na hakuna Mtanzania ambaye niliwahi kumtuma hicho kitu kimetengenezwa kwa nia ya kunichafua.

RADIO: Mheshimiwa unatafsiri vipi tukio hili?

AZZAN: Mimi ninachotafsiri tayari mapambano ya 2015 ndiyo yanaanza na watu wanatafuta jinsi ya kunichafua sababu hata tukienda kwenye kura nitawashinda, lakini si kutafuta mbinu chafu za kunichafua.

Yapo maneno ambayo nayazungumza bungeni hayawafurahishi wengine, lakini kwa Watanzania wengi yana manufaa, kwa hiyo kwa wale ambao hayawafurahishi wanaweza wakawa wamechangia katika kunichafua.

RADIO: Lakini Mheshimiwa Idd Azzan mara nyingi tu umekuwa ukitajwa na watu mbalimbali kwamba unajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya ama wewe ni mmoja kati ya watu wanaowaagiza watu mbalimbali kusafirisha mizigo hiyo ya dawa za kulevya hilo kwa upande wako unalizungumza vipi.

AZZAN: Nasema binafsi nimejipeleka polisi na nilishajipeleka mara ya kwanza baada ya kutokea tuhuma kama hizi, nikawaambia polisi wafanye uchunguzi kama nahusika nichukuliwe hatua za kisheria, nimekwenda tena kuwaambia polisi na nasisitiza polisi wafanye uchunguzi wa kina kama nahusika hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yangu.

Kama nitabainika nahusika na biashara hiyo niko tayari kupigwa risasi hadharani, lakini pia sitendewi haki kwa wale ambao wanazusha jambo hili wachukuliwe hatua za kisheria.

RADIO: Lakini Mheshimiwa kwa upande mwingine tayari taarifa zimeshatolewa kama hivyo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, sasa endapo itabainika kweli umehusika ama hujahusika ni kitu gani ambacho utakifanya.

AZZAN: Naomba niweke wazi kama itathibitika ninamtuma mtu madawa ya kulevya kupitia bandari gani mimi nipo tayari kuhukumiwa sababu sipo juu ya sheria na pia nipo tayari niwekwe hadharani waninyonge sifai kuendelea kuwapo Tanzania kama nahusika na hilo, na kama sihusiki serikali initendee haki kwa watu wanaosambaza uvumi huu nao wachukuliwe hatua siyo wakae tu na kumrushia mtu vitu vya uongo.

Awali Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato akihojiwa katika kipindi hicho juu kwanini JNIA umeonekana kuwa kitovu cha kupitishia dawa za kulevya, alisema sababu kubwa ni kwamba kuna tofauti kati ya nchi na nchi katika masuala ya teknolojia katika kubaini dawa za kulevya.

Kamanda Kato alisema nchi nyingine wana vifaa vya kisasa zaidi na kwamba wakati sasa umefika kwa serikali kuwekeza katika kupata vitendea kazi zaidi ili kufanikisha mapambano ya dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa wamekuwa wakishirikiana na viwanja vingine vya nchi mbalimbali kwa kubadilishana taarifa lengo likiwa ni mapambano ya biashara hiyo.

“Kimsingi wanaokamatwa wanakuwa ni wabebaji tu na siyo matajiri wa dawa za kulevya, bahati mbaya wabebaji wamekuwa wagumu sana kutoa ushirikiano kwa polisi, nasisitiza vitendea kazi vinachangia kuponya mtu asikamatwe nchini na kwenda kukamatwa nje,” alisema.

Kamanda Kato alisema katika kipindi cha miezi sita hadi nane watu 14 wamekamatwa wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya nchini.

Julai 5, mwaka huu wasichana wawili, Agnes Jerald (25) na Melisa Edward (24), walipita JNIA na shehena ya dawa za kulevya kilo 150 na walikamatwa Afrika Kusini na kushtakiwa nchini humo kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya.

Hawa walikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo wakiwa na shehena ya dawa hizo aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8.

Ijumaa wiki iliyopita yaani Julai 26, mwaka huu, Watanzania wengine wawili, walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hong Kong.

Taarifa kutoka Hong Kong za Ijumaa wiki iliyopita zinaeleza kwamba, maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Hong Kong (HKIA), walimkamata kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26 akitokea Tanzania na alikuwa na dawa za kulevya aina ya heroine kilo 1.6 zenye thamani ya Sh. bilioni 1.5, kwenye mzigo wake wa mkononi.

Siku hiyo hiyo jioni, maofisa hao walimkamata Mtanzania mwingine mwenye miaka 45 ambaye alipelekwa hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa za kulevya aina ya heroine. Taarifa zaidi zilieleza kuwa Mtanzania mwingine mwenye miaka 28 alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine.

Source: Nipashe.