Showing posts with label Siasa. Show all posts
Showing posts with label Siasa. Show all posts

Wednesday, July 2, 2014

Serikari kutaifisha mashamba yasiyoendelezwa Tanga.


Waziri mkuu mheshimiwa Mizengo Pinda ameuagiza uongozi wa serikali mkoa wa Tanga kuorodhesha mashamba yote yasiyoendelezwa kisha kuwasilisha kwake ili aweze kumkabidhi mheshimiwa Rais aweze kutoa maamuzi kufuatia baadhi ya wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa na kusababisha wananchi kukosa mashamba ya kulima.
Mheshimiwa Pinda ametoa agizo hilo wakati akihutubia mamia ya wakazi wa mkoa wa Tanga katika kilele cha maonesho ya biashara ya halmashauri zote nchini yaliyofanyika kitaifa jijini Tanga kisha washindi kukabidhiwa tuzo kama ishara ya kuvutia wawekezaji.
 
Kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu ujao waziri Pinda amewaagiza viongozi wa kuanzia serikali za mitaa na vijiji,kata,tarafa hadi wilaya na taifa kwa ujumla kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuchagua viongozi wenye sifa katika uchaguzi mkuu ujao wa serikali za mitaa ili kulinda Demokrasia ya kweli kwa watanzania.
 
Awali mwenyekiti wa jumuiya ya tawala za serikali za mitaa nchini (ALAT) Dr,Didas Masaburi amesema jumuiya haitamuunga mkono mgombea kuanzia ngazi ya Rais,Ubunge na Diwani endapo atashindwa kusimamia mchakato wa ugatuaji madaraka kwenda kwa wananchi ili kuleta demokrasia ya kweli.
 
Katika hitimisho la maonesho ya biashara ya halmashaurio zote nchini waziri mkuu alitoa zawadi kwa washiriki washindi wa maonesho hayo ambayo halmashauri ya jiji la Tanga iliibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na halmashauri ya Bukoba.

Tuesday, July 1, 2014

Serikali inaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa


Waziri Mkuu MIZENGO PINDA amesema serikali inaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza mkoani TANGA na mameya wa majiji, manispaa na wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya nchini, Waziri Mkuu PINDA amesema hata hivyo hatma ya kufanyika kwa uchaguzi huo inategemea kukamilika kwa mchakato wa Katiba mpya.

Waziri Mkuu amesisitiza suala la ukusanyaji mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali na kuongeza kuwa amewaandikia barua Wakuu wa Mikoa akiwataka waweke utaratibu wa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu juu ya makusanyo ya kila Halmashauri zilizo kwenye mikoa yao.

Halmashauri zote zaagizwa kuendelea na matayarisho ya uchaguzi


 Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ameziagiza halmashauri za wilaya nchini kuendelea na matayarisho ya uchagauzi mkuu wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu huku jitihada zikifanywa na serikali kuwaomba umoja wa katiba ya wananchi  -Ukawa kukubali kuridhia ombi la kurudi bungeni ili azma hiyo iweze kufikiwa.

Mheshimiwa Pinda ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakurugenzi, wenyeviti na viongozi wa serikali ngazi ya taifa katika kikao cha pamoja kilichofanyika jijini Tanga.
Amesema kama kutakuwa na mabadiliko kuhusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo huku pande zote mbili zikirudi kuendelea na bunge la katiba viongozi hao watapewa taarifa kuhusu mchakato huo lakini matayarisho ya uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa ni lazima yafanyike.
Kuhusu uwekezaji waziri mkuu ameziagiza halmashauri za wilaya nchini kuhakikisha kuwa wanatangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo yao kama walivyofanya mkoa wa Tanga mwishoni mwa mwaka jana ambapo walifanya kongamano la uwekezaji lililoshirikisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi hatua ambayo imeanza kuleta mafanikio kwa Tanga na taifa kwa ujumla.

Monday, August 5, 2013

JAJI FRANCIS MUTUNGI ATEULIWA KUWA MSAJILI MPYA WA VYAMA VYA SIASA...TENDWA KWA HERI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji Francis S.K. Mutungi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Taarifa iliyotolewa Dar Es Salaam leo, Jumatatu, Agosti 5, 2013, na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza Ijumaa iliyopita Agosti 2, 2013.

Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. John Tendwa ambaye amestaafu Utumishi wa Umma kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, DAR ES SALAAM.

SITTA "WABUNGE VITI MAALUMU HAWANA UMUHIMU WOWOTE"


Wiki moja baada ya kukaririwa akisema baadhi ya wabunge wa CCM ni mizigo na kwamba hawana mchango wowote bungeni na wala hawatembelei majimbo yao wakisubiri kubebwa na chama, Spika wa Bunge wa zamani, Samuel Sitta amewageukia wabunge wa Viti Maalumu akisema hawana umuhimu wowote.

Akizungumza kwa simu juzi, Sitta ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema: “Ninakerwa sana na mfumo wa Viti Maalumu, kwanza sioni umuhimu wa mfumo huu kuendelea kuwepo katika Katiba Mpya. Hawana umuhimu wowote.”

Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Busega Mkoa wa Simiyu Julai 29, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuimarisha uhai wa chama, Sitta aliwajia juu bila ya kuwataja baadhi ya wabunge wa CCM.

“Wanakwenda bungeni hawachangii, hawana hata hoja za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo,” alisema Sitta na kuongeza: “Wapo baadhi ya wabunge, hawajawahi hata siku moja kwenda kwenye majimbo yao kuwatembelea wananchi waliowachagua... Inawezekana hata wapiga kura wakawa wamewasahau. Hawa hawafai hata kuchaguliwa wakiomba tena kura.”

“Rais Jakaya Kikwete amejitahidi sana kuleta mabadiliko, ameleta mafanikio ya uchumi na mambo mengi. Inatakiwa wabunge waende wakawaeleze wananchi maendeleo haya, inawezekana hawayajui lakini watu hawaendi jimboni, wananchi watayafahamu vipi haya maendeleo?”

Juzi, akizungumzia wabunge wa Viti Maalumu, Sitta alisema... “Wengi wao hawachangii chochote na mbaya zaidi hakuna wa kuwahoji chochote kama wabunge wanavyorudi jimboni.

“Ikifika wakati wa posho wapo. Sisemi kama naumia wao kuchukua posho.... hawa wanachukua posho wanawajibika kwa nani? Nani anahoji utendaji wao na zaidi itakapokuja Katiba Mpya ya kuwawajibisha wabunge wazembe, hawa watawajibishwa wapi?”

“Rasimu ya Katiba Mpya isiwaruhusu hawa... hawa nao ni mzigo mwingine. Wakifika bungeni hawachangii chochote, hawawezi kuwajibishwa na yeyote kwa mfumo uliopo na pia hawawajibiki popote, sasa huu si mzigo?”

Walikwishaanza mkakati

Hata hivyo, Juni 9, mwaka huu, ikiwa ni wiki moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kutangaza Rasimu ya Katiba huku ikifuta Viti Maalumu, wabunge wanawake walianza kuweka mikakati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa lengo la kukamata majimbo.

Kwa mara ya kwanza, wabunge hao wa Viti Maalumu walikutana kwa siku mbili kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa, Dodoma lengo likiwa ni kujadili mikakati mbalimbali ya kupambana jimboni.
Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake, Anna Abdallah alisema wanaweka mikakati kuwawezesha kusimama wenyewe kwenye majimbo mwaka 2015 hasa baada ya kufutwa kwa Viti Maalumu katika rasimu.

Mbunge huyo alikiri kuwa Viti Maalum haviwapi sifa stahiki kama wabunge kwa kuwa hawana uwakilishi wa moja kwa moja kwa wananchi. Alisema bila kuangalia nafasi za vyama, suala la Viti Maalumu linawabagua na wabunge wa majimbo.

Msimamo wa wabunge wa Viti Maalumu

Baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutangaza rasimu, baadhi ya wabunge wa Viti Maalumu walizungumzia hatima ya nafasi hiyo huku wengi wakionekana kuunga mkono kufutwa kwake.
Mmoja wao ni Grace Kihwelu (Chadema), ambaye alisema: “Ninachotaka wabunge twende hukohuko jimboni tukapambane kwani inaleta heshima. Hii ya kuteuliwa inatunyima raha.”

Mbunge mwingine wa Chadema kutoka Zanzibar, Mariam Msabaha alisema: “Mimi nilikuwa wa kwanza kupingana na haya ya Viti Maalumu ndiyo maana nikasimama moja kwa moja Jimbo la Jang’ombe kupigana. Sikutaka kuteuliwa.”

Catherine Magige (CCM), alisema: “Viti Maalumu havionyeshi ufanisi wa moja kwa moja na sehemu kubwa mbunge ndiye anayeonekana kwa wananchi.”

Mbunge mwingine wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata alisema mfumo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba utarudisha heshima kwa wabunge wanawake kwa kuwa wanakwenda kupambana katika majimbo.
Ritha Kabati wa CCM alielezea kufurahishwa kwake na Tume ya Warioba kuondoa Viti Maalumu... “Vilikuwa vinatudhalilisha, watu walikuwa hawatupi thamani halisi kama wabunge.”
Suzan Lyimo wa Chadema alisema: “Nimeupenda uamuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wakati mwingine Viti Maalumu vilikuwa vinatolewa kwa rushwa na sisi wanawake ndiyo ilikuwa inasemwa vibaya. Sasa ni bora huko katika majimbo tukapambane.”

Source: Mwananchi

Sunday, August 4, 2013

DIWANI CHADEMA AFICHUA NJAMA ZA CCM.


DIWANI wa kata ya Turwa katika Halmashauri ya mji wa Tarime wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Charles Ndessi Mbusiro, amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), wilayani Tarime, kimepora uwanja wa michezo bila ridhaa ya wananchi. 

Diwani huyo alitoa tuhuma hizo juzi wakati alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa Tarime waliohudhuria maadhimisho ya miaka mitano ya kifo cha aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Chacha Zakayo Wangwe.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Serengeti, diwani huyo alisema kuwa uwanja huo ni mali ya wananchi wote wa Tarime lakini CCM kwa hila zake wameupora.
“Baada ya kuona uwanja huo ukitumiwa mara kwa mara na CHADEMA katika mikutano yake, wamefanya ujanja na kupata hati ambapo sasa wanadai kuwa ni mali yao.

“Ndugu zangu wananchi wa Tarime napenda kuwafahamisha kuwa uwanja huu sasa ni wa CCM, wamefanya njama na wameuchukuwa na wanadai kuwa ni wa kwao na tayari wanataka kujenga vibanda na wameshagawana vibanda kila kiongozi ana milango yake sijui kama wananchi mnalijua hilo?’’ alisema na kuhoji diwani huyo.

Diwani huyo alidai kuwa uwanja huo ulijengwa na wananchi wote kipindi cha mfumo wa chama kimoja na kwamba CCM haina hati miliki wala haina mamlaka ya kuupora.

Aliwabana viongozi wa CCM wawaambie wananchi kama chama chao ni cha biashara au ni chama cha siasa kwani viongozi wa chama hicho ndio waliojipanga kufanya biashara katika uwanja huo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa mji wa Tarime wamedai kusikitishwa na kitendo hicho ambacho walisema ni cha kifisadi na kwamba jambo hilo si la kufumbia macho.

“Unajua hawa watu wa ‘magamba’ wamezoea sana dhuluma na ufisadi; hiki kiwanja ni cha wananchi wote na wala si cha CCM sasa leo nimeshangaa kusikia kuwa wamekichukua kwa nguvu ili kiwe mali yao kwa kweli halitawezekana, tumechoka kuonewa liwalo na liwe lazima wakirudishe" alisema mwananchi mmoja Mwita Mseti mkazi wa mtaa wa Rebu.

CHADEMA SASA YAPOTEA, DR. SLAA AWAUNGA MKONO WAASI WA KONGO ....AMSHANGAA KIKWETE KWA KUMWINGILIA KAGAME


Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, amemkosoa Rais Jakaya Kikwete, kuhusu kauli yake ya kumshauri Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuzungumza na waasi wa serikali yake ...

Dk. Slaa amesema haoni busara kwa Rais Kikwete kuwaambia viongozi wa Rwanda, akiwamo Rais Kagame, kuzungumza na wafuasi wa chama cha FDRL walioko Congo.

Slaa aliyasema hayo wakati akizungumza katika kongamano la vijana wa Chadema (BAVICHA) la uchumi na ajira lililofanyika jana jijini Dar es Salaam.

“Rais Kikwete hapa nyumbani hawezi kuzungumza na wapinzani na hajachukua hatua dhidi ya wauaji wa mwandishi Daudi Mwangosi...

"Alishauriwa amuwajibishe Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda na badala yake amempandisha cheo,” alisema Slaa.

Kauli Dk Slaa imekuja siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kuwa Tanzania haina mgogoro na nchi ya Rwanda, kutokana na kauli za kejeli na matusi zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa nchi hiyo dhidi yake na Tanzania.

Kumezuka sitofahamu ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda, baada ya Rais Kikwete kuitaka Rwanza imalize ugomvi na waasi kwa njia ya mazungumzo ya amani...

Rais Kikwete aliutoa ushauri huo wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia hivi karibuni.

Ushauri huo ulionekana kumchukiza Rais Kagame, anayedaiwa kuhutubia mikutano kadhaa nchini kwake na kutumia lugha ya matusi, kejeli na dhihaka dhidi ya Rais Kikwete na Tanzania.
Kitendo cha Dr Slaa kumkingia kifua Kagame kinatia shaka uzalendo wake na chama chake kwa taifa hili ...

Sote tumekuwa tukishuhudia matusi ya Kagame dhidi ya Tanzania.Iwaje Rais Kikwete aonekane mbaya kwa kumjibu Kagame, tena kwa lugha ya kizalendo??

Kagame amekuwa akituhumiwa na jumuiya mbalimbali za kimataifa kwa kutoa misaada ya kivita kwa waasi wa M23 ambao wamekuwa wakiua raia na kuwabaka wanawake....

Kauli ya Dr Slaa ina mambo mengi yaliyojificha na huenda yeye na chama chake ni wafuasi wa karibu wa M23 kama ilivyo kwa Kagame.

Kuwa mpinzani, haimaanishi ukosoe kila kitu.

Saturday, August 3, 2013

MWIGULU NCHEMBA: CHADEMA wanatafuta umaarufu kupitia jina langu


Kumekuwepo na jitihada za makusudi za chadema, baadhi ya magazeti yanayofanya kazi ya uenezi ya chadema na wafuasi wa chadema kufanya kila njama kunichafulia jina kwa sababu na manufaa yao wayajuayo wenyewe.

1) Leo (Alhamisi) wameibuka na kihoja kuwa Dr Slaa hatarini, wameweka na picha yangu. Hivi mimi nihangaike na Dr Slaa wa nini? Kwanza mimi ndio naanza siasa, na yeye ndio anamaliza, in no way he is a threat to me.

I do not find him a competitor and he cant halt my political ambitions. Wengine wanadiriki kumpima slaa namimi, huyu sio saizi yangu na yeye anajua, hana kipaji and and he is outdated.

Am 38 yrs old and he is around 70 years, WHO WAS SLAA WHEN HE WAS AT THE AGE OF 38 yrs (my age), no body. WHERE WILL I BE 2YEARS TO
10 YEARS FROM NOW?

KAMA SASA TU CHADEMA NZIMA KUANZIA MAKAO MAKUU MPAKA VIJIWEN KWAO agenda ni MWIGULU, MWIGULU.? YOU PEOPLE TAIFA HILI LINA MASWALA MENGI YA MHIMU, STOP MAKING MWIGULU AN AGENDA FOR YOUR PARTY.

2) Majuzi hivi bila aibu mkasema Mwigulu anahusika na kulipua bomu mkutano wenu,kisa Nilikwepo Arusha. May 5 pia nikiwa Ethiopia kuna bomu lililipuliwa hapohapo ars mbona hamlisemi nani alilipua hilo.
Zote hizi ni jitihada za kufunika uovu wenu mkidhani kwa kuwa nawasema kuhusu ugaidi wenu basi mkigeuza kibao nitaacha. IT IS NEITHER MY NATURE NOR MY CHARACTER TO BE AFRAID.

This won't stop me, subirini kesi ianze watanzania watawajua cos mtu wenu alikiri kila kitu ninyi mnacheza na akili za watu tu kwa propaganda kwa manufaa ya kisiasa.

Eti anavaa kofia ya china na bomu lilitengenezewa china hivyo anaweza kuwa mhusika. What a myopic statement? Mbona simu za kichina mnazo? Zinauhusiano na mabomu?

3) Red Brigade nayo mmeshindwa kusema kwanini MKT wenu alisema hamtategemea polisi wala Jeshi la wananchi? Hii ndio tofauti na greenguard, badala yake hoja imekuwa Mwigulu mpaka mnatengeneza na picha za kuunga.

4) Hata mkanda ule mnasema nilimpanga mtu arekodi mazungumzo, sawa, je nilimpagia na kiongozi wenu aseme yale aliyoyasema? Au hata hamjui alisema nini? Cos alishakiri yote kwenye maelezo yake polisi, je nilimpanga naye aseme yale ili arekodiwe?

Hivi vijana wa chadema nani kawaroga? Mpaka you a missing even such a plain fact. Be informed that God has a complete plan of my life. You can not tarnish or halt it. I will move from Glory to Glory.

TUTAHESHIMIANA TU.

Friday, August 2, 2013

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA WANANCHI, TAREHE 31 JULAI, 2013


Utangulizi

 Ndugu wananchi;
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kwa mara nyingine tena kutekeleza utaratibu wetu huu mzuri tuliojiwekea wa Rais kuzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi.

Ndugu Wananchi;
Mwezi Julai, 2013 ulikuwa wa neema kubwa ya wageni kwa nchi yetu wakiwemo watu na viongozi mashuhuri duniani. Natoa shukrani nyingi kwa Watanzania wenzangu kwa jinsi tulivyowapokea wageni wetu zaidi ya 1,700. Wamefurahi kuwepo kwao nchini na wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu. Wageni wetu wamekuwa wa manufaa makubwa kwa nchi yetu. Wamesaidia kuitangaza Tanzania duniani na kuendeleza fursa za kukuza utalii, biashara na uwekezaji nchini na kwingineko katika Afrika.

Mkutano wa Smart Partnership

Ndugu wananchi;
Wageni wetu wa kwanza ni wale waliokuja kuhudhuria Mkutano wa Global 2013 Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni hadi 1 Julai, 2013. Mkutano huo ulihudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka mabara yote duniani wakiwemo Watanzania. Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na wakuu wa nchi na Serikali, viongozi wastaafu, wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika na taasisi za kimataifa, makampuni ya ndani na nje, wafanyabiashara, wasomi, asasi za kijamii na watu wa makundi mbalimbali katika jamii. Makampuni yetu 21 nayo yaliungana na makampuni mengine 28 kutoka nje ya nchi kushiriki kwenye maonesho ya matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika sambamba na mkutano huo.

Ndugu Wananchi;
Agenda kuu ya majadiliano ya mwaka huu ilikuwa ni “Matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi Barani Afrika (Leveraging Technology for Africa’s Social-Economic Transformation: The Smart Partnership Way). Tuliichagua mada hii kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa matumizi ya sayansi na teknolojia ndiyo chachu kubwa iliyoleta mageuzi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi. Ndiyo siri ya mafanikio katika nchi zilizoendelea na zinazopiga kasi kubwa ya maendeleo duniani.

Bahati mbaya sana kumekuwa na maendeleo na matumizi madogo ya sayansi na teknolojia katika Afrika. Ndiyo maana nchi za Afrika ziko nyuma kimaendeleo ukilinganisha na zile zilizoendelea. Katika mkutano huo umuhimu wa kuendeleza na kuongeza matumizi ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya maendeleo Barani Afrika ulitambuliwa na kusisitizwa.

Mkutano ulihimiza na kusisitiza kuwa sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya nchi za Afrika zitoe kipaumbele kwa kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia. Nchi zetu zimehimizwa kuwekeza katika elimu ya sayansi na teknolojia pamoja na kujenga uwezo wetu wa ndani wa uvumbuzi, ubunifu, umiliki na uendelezaji wa sayansi na teknolojia. Aidha, imesisitizwa kwa nchi zetu ziongeze kasi ya kutumia sayansi na teknolojia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kuongeza ufanisi na kasi ya maendeleo.

Ndugu Wananchi;
Jambo la kutia faraja kwetu nchini ni kwamba mambo yote hayo tunayafanya. Tunachotakiwa sasa ni kufanya vizuri zaidi na kuongeza uwekezaji na kasi ya kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Tutaendelea kuboresha sera, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kwa ajili ya maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.

Ziara ya Rais wa Marekani Nchini Tanzania

Ndugu wananchi;
Mgeni wetu wa pili alikuwa Rais wa Marekani, Mheshimiwa Barack Obama, aliyefanya ziara nchini kwetu kati ya tarehe 1 - 2 Julai, 2013. Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Marekani na Tanzania. Kama mjuavyo, nchi zetu mbili zina uhusiano wa kibalozi tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mwaka 1964.

Uhusiano wetu umepita katika vipindi mbalimbali na kwamba hivi sasa umekuwa mzuri zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi zetu mbili. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la misaada ya maendeleo kutoka Marekani na uwekezaji wa vitega uchumi na biashara navyo vinakua. Pia ziara za kiserikali za viongozi wa nchi zetu kutembeleana zimeongezeka. Kama mtakavyokumbuka, mwaka 2008 aliyekuwa Rais wa Marekani Mheshimiwa George W. Bush alifanya ziara ya siku nne nchini. Pia Mawaziri mbalimbali wa Serikali ya Marekani wametembelea Tanzania akiwemo Mheshimiwa Hilary Clinton akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyekuja mwaka 2011.

Ndugu Wananchi;
Nchi ya Marekani imekuwa mshirika wetu muhimu wa maendeleo katika nyanja mbalimbali. Kwa upande wa afya kwa mfano, tunapata msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya malaria na UKIMWI. Katika maendeleo ya elimu, nako wanatusaidia katika mafunzo ya wataalamu mbalimbali pamoja na upatikanaji wa vitabu vya sayansi na hisabati kwa ajili ya shule za sekondari. Kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia, Marekani inatusaidia katika kuimarisha miundomuinu ya barabara, umeme na maji. Ujenzi wa barabara za Tanga – Horohoro, Namtumbo – Songea – Mbinga; Tunduma – Sumbawanga na baadhi ya barabara za Pemba, ujenzi wa njia ya pili ya kupeleka umeme Unguja kutoka Dar es Salaam, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na usambazaji wa umeme katika Mikoa 10 ya Tanzania bara ni miongoni mwa matunda ya msaada wa Mfuko huo. Pamoja na hayo, ipo miradi ya kuongeza maji katika jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Morogoro ambayo inaendelea kutekelezwa.

Ndugu Wananchi;
Wakati wa ziara yake, Rais Obama alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali yake ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu. Alielezea kuridhika na hatua tuliyofikia ya kukuza demokrasia nchini, utawala bora na kuwekeza katika maendeleo ya watu wetu. Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zetu. Katika hili ameahidi kuongeza misaada ya maendeleo na kiufundi katika sekta za afya, elimu, kilimo, barabara, nishati na maendeleo ya vijana. Pia, alithibitisha kwamba nchi yetu itaendelea kunufaika na ufadhili wa Awamu ya Pili ya Mfuko wa Changamoto za Millenia. Katika awamu hii, maeneo yatakayopewa kipaumbele hapa kwetu ni umeme na barabara za vijijini. Mazungumzo ya miradi itakayotekelezwa katika awamu hiyo yanaendelea vizuri.

Power Africa

Ndugu Wananchi;
Rais Obama alitumia fursa ya ziara yake nchini kuzindua mpango wa Serikali yake wa kusaidia maendeleo ya sekta ya umeme katika Bara la Afrika. Mpango huu unaoitwa “Power Africa Initiative” umetengewa kiasi cha dola za Marekani bilioni 7 na Serikali ya Marekani na makampuni binafsi ya nchi hiyo yameahidi kuwekeza dola bilioni 9 katika mpango huo. Kwa kuanzia, nchi sita za Afrika (Ethiopia, Ghana, Nigeria, Tanzania, Liberia na Kenya) ikiwemo Tanzania zitahusishwa.

Bila ya shaka Mpango huo ukikamilika utasaidia sana kuimarisha upatikanaji wa umeme barani Afrika ambayo ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ni ukweli ulio wazi kuwa ukosefu wa umeme wa kutosha na wa uhakika ni sababu kubwa inayokwamisha maendeleo ya haraka katika nchi za Afrika. Hivyo basi, msaada huu ni muhimu sana kwetu. Kwa ajili hiyo nimeagiza Wizara ya Nishati na Madini iandae mkakati madhubuti wa namna Tanzania itakavyoshiriki na kufaidika na mpango huo. Nataka mpango huo utakapoanza kutekelezwa utukute sisi tupo tayari kutumia fursa zake.

Vile vile, ndugu wananchi, katika ziara hiyo Rais Obama alielezea nia ya Serikali yake kutaka kuwepo mpango wa kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji baina ya nchi yake na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nimeelekeza Wizara husika yaani Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko nao watengeneze mkakati utakaoonesha jinsi tulivyojipanga kufaidika na mpango huo. Lazima tujiandae vyema na mapema tunufaike saiwa na mpango huo.

Ziara ya Rais Mstaafu wa Marekani Nchini

Ndugu Wananchi;
Sambamba na ziara ya Rais Obama, nchi yetu ilipata bahati ya kutembelewa tena na Rais Mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush na mkewe Laura Bush, tarehe 1 hadi 3 Julai, 2013. Kwa udhamini wa asasi ya George W. Bush Foundation waliandaa Mkutano wa Wake wa Marais wa Afrika uliofanyika hapa Dar es Salaam, tarehe 2 na 3 Julai, 2013. Mama Michelle Obama naye alishiriki mkutano huo uliozungumzia kuimarisha maendeleo na afya ya wanawake Barani Afrika.

Katika mkutano huo, pia, Mheshimiwa George W. Bush alizindua mpango wa kuimarisha mapambano dhidi ya kansa ya shingo ya kizazi na matiti barani Afrika. Kufuatia Mpango huo, Serikali ya Marekani imetoa dola milioni 3 na mashine 16 za Cryo Therapy zinazotumia baridi kali kuua chembechembe za kansa. Msaada huo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa kila mwaka hapa nchini zaidi ya Watanzania 21,000 wanapata maradhi ya kansa. Kati ya hao asilimia 29.4 ni wanawake wanaopata magonjwa ya kansa ya shingo ya uzazi na asilimia 6.2 wanapata kansa ya matiti. Naamini Mpango huu utatusaidia sana katika kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi haya yanayowasumbua na kuua kina mama wengi nchini. Nimeitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka utaratibu mzuri ili msaada huo utumike ipasavyo na kuwanufaisha walengwa.

Ziara ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Nchini

Ndugu Wananchi;
Tarehe 23 mwezi Julai, 2013 pia tulitembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Mheshimiwa Tony Blair. Katika mazungumzo yetu Mheshimiwa Blair aliahidi kuisaidia nchi yetu kupitia taasisi yake ya Africa Governance Initiative kusaidia kusambaza umeme wa jua katika shule zetu za sekondari vijijini, maboresho ya shirika letu la umeme (TANESCO) na kusaidia uanzishaji na uimarishaji wa Kitengo cha Rais cha Ufuatiliaji Utekelezaji wa Programu za Maendeleo (Presidential Delivery Bureau - PDB). Tunamshukuru kwa ahadi yake hiyo itakayochangia katika jitihada za kujiletea maendeleo.

Ziara ya Waziri Mkuu wa Thailand Nchini

Ndugu Wananchi;
Tarehe 30 Julai, 2013 tulimpokea Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, Waziri Mkuu wa Thailand aliyefanya ziara ya siku tatu nchini. Lengo la ziara yake ni kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Thailand na Tanzania. Katika ziara hiyo, tumezindua Jukwaa la Wafanyabiashara wa Thailand na Tanzania (Thai-Tanzania Business Forum) ili kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu. Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra alitumia fursa hiyo kufafanua sera ya Thailand kwa Afrika inayosisitiza kukuza ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na kibiashara. Pia amepata nafasi ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea mwenyewe jinsi nchi yetu ilivyobarikiwa kwa kuwa na kivutio hicho cha aina yake. Alipokuwa kule nchi zetu zilitiliana saini maelewano ya ushirikiano katika kulinda na kuhifadhi wanyama pori.

Katika mazungumzo yangu na yeye, tumekubaliana kuchukua hatua thabiti kukuza ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Tumetiliana saini mikataba mitano ya ushirikiano kwa mambo yafuatayo: Kukuza na kulinda vitega uchumi; kubadilishana wafungwa; ushirikiano wa kiufundi; na ushirikiano kwa masuala ya madini. Aidha, Waziri Mkuu huyo ameahidi kuwahimiza wawekezaji wa nchini mwake kuja Tanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo kilimo, utalii, viwanda nakadhalika. Pia, Waziri Mkuu wa Thailand ameahidi kuwa Serikali yake itatoa ufadhili kwa vijana 10 kusoma Shahada ya Uzamili nchini humo. Vile vile, nchi hiyo itaanza kuleta wataalamu wa afya wa kujitolea kuja kushirikiana na wataalam wetu kuimarisha huduma ya afya nchini.

Ziara hizi zinaonesha utayari wa dunia kuunga mkono jitihada zetu za kujiletea maendeleo. Naomba Watanzania wenzangu tutumie vizuri utayari huo wa dunia kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Tusijikwaze wenyewe.

Ziara ya Kagera

Ndugu wananchi;
Kuanzia tarehe 24 hadi 29 Julai, 2013, nilifanya ziara Mkoani Kagera. Nilishiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa na kuzindua jengo jipya la Mahakama Kuu. Pia niliweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba na kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara za Kigoma – Lusahunga na Kyaka – Kayanga – Bugene. Vile vile nilizindua Wilaya mpya ya Kyerwa na kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuona na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ili kuzitafutia majawabu.

Sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa zilifana sana. Niliwapongeza viongozi wa Jeshi na wa Mkoa kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizo. Pia nilirudia kumpongeza Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, kwa uamuzi wake wa busara wa kufanya sherehe za kumbukumbu za mashujaa wetu pale Kaboya badala ya kufanyikia Dar es Salaam tu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Ni uamuzi muafaka na wa busara kwani pale Kaboya ndipo walipolala mashujaa wetu waliopoteza maisha yao kutetea mipaka na uhuru wa nchi yetu dhidi ya Nduli Iddi Amin. Hali kadhalika, kule Naliendele, Mtwara ambapo sherehe za mashujaa zilifanyika mwaka wa juzi, ndipo walipozikwa mashujaa wetu waliopoteza maisha kuisaidia nchi jirani na rafiki ya Msumbuji kutetea Uhuru wake dhidi ya wakoloni, makaburu na vibaraka wao wa ndani ya Msumbiji.

Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu pale Kaboya niliwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba katika kuwakumbuka mashujaa wetu wale na sisi tulio hai, hatuna budi kutambua wajibu wetu wa kuwa tayari kujitolea muhanga kwa ajili ya kulinda uhuru wa mipaka ya nchi yetu. Nilisisitiza utayari wa nchi yetu kulinda mipaka yake na kwamba mfano wa mashujaa waliolala pale ni fundisho kwa mtu ye yote anayetamani kumega kipande cho chote cha ardhi ya nchi yetu. Atakiona cha mtema kuni kilichomkuta Nduli Iddi Amini au hata zaidi.

Nimesikia kuwa kauli yangu ile imetafsiriwa visivyo na kupotoshwa na baadhi vyombo vya habari na hata majirani zetu. Tafsiri hizo ni potofu. Sikumtaja mtu ye yote au nchi yo yote. Nilikuwa nazungumzia wajibu wa majeshi yetu na raia wa nchi yetu wa kulinda uhuru na mipaka yetu na kwamba hatutamruhusu mtu au nchi yo yote kutupokonya wala kuichezea haki yetu hiyo ya msingi. Tuko tayari kuitetea hata kama gharama yake ni maisha yetu kama walivyofanya mashujaa waliolala Kaboya.

Mahakama Kuu

Ndugu Wananchi;
Katika ufunguzi wa Mahakama Kuu ya Bukoba nilisisitiza dhamira na utayari wa Serikali yetu kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kuwa na Mahakama Kuu katika kila Mkoa. Baada ya kukamilika kwa Mahakama Kuu ya Bukoba bado kuna Mikoa 14 hainazo. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 tumetenga fedha za kujenga Mahakama Kuu katika Mikoa 7 na nilirudia ahadi yangu kuwa katika mwaka ujao wa fedha tutatoa fedha za kumalizia Mikoa 7 iliyosalia. Niliamua tuongeze kasi ya kujenga Mahakama Kuu hizo ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kutimiza ipasavyo wajibu wake wa kutoa haki nchini.

Maendeleo ya Mkoa wa Kagera

Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa Kagera nilifurahishwa na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Taarifa za Mkoa na Wilaya zimefafanua kwa kina mambo mazuri yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika Mkoani. Wameelezea furaha yao kwa mafanikio yaliyopatikana ambayo baadhi nimeyashuhudia au hata kushiriki kuyazindua na kuweka mawe ya msingi. Taarifa hizo pia zimelezea mambo mengi zaidi wanayotaka yafanyike na matatizo mapya na hata ya zamani ambayo wanataka yapatiwe ufumbuzi.

Katika mazungumzo yangu na viongozi na wananchi, yapo mambo ambayo yako kwenye uwezo wao kijijini, Wilayani na Mkoani kuyapatia ufumbuzi. Tulikubaliana na kuelekezana nini kifanyike. Yapo mengine mengine ambayo yanahitaji nguvu ya taifa tumeyachukua kuja kuyafanyia kazi. Kuna baadhi yaliwahusu Mawaziri ambao nilikuwa nao ziarani waliyasemea na kuyafanyia kazi palepale yalipojitokeza.

Ulinzi na Usalama

Ndugu Wananchi;
Kuna mambo matatu yahusuyo usalama ambayo yalizungumzwa na wananchi kwa uchungu mkubwa ambayo niliamua tuyashughulikie kitaifa. Mambo hayo ni ujambazi wa kutumia silaha kuteka magari, kupora mali na watu kuuawa. Jambo la pili ni wahamiaji kutoka nchi jirani wanaoingia, kuishi na kufanya shughuli nchini kinyume cha sheria. Na tatu, mifugo kuingizwa kwa wingi nchini bila kufuata taratibu husika na mingine kuingizwa katika hifadhi za wanyama.

Ndugu wananchi;
Nilitoa maagizo kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Uhamiaji watengeneze mpango kabambe wa kuyashughulikia matatizo hayo. Watayarishe na kutekeleza operesheni maalum itakayo au zitakazokomesha ujambazi, kuondoa wahamiaji wasiokuwa halali na kuondoa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume na utaratibu na ile iliyoko kwenye maeneo yasiyo stahili.

Aidha, niliwataka majambazi wajisalimishe na wasalimishe silaha zao ndani ya wiki mbili na siku hizo zinaanzia tarehe 29 Julai, 2013 nilipomaliza ziara yangu Mkoani humo. Kwa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria nimewataka watumie muda huo kuondoka nchini au kuhalalisha ukaazi wao. Hivyo hivyo kwa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume na sheria au ile iliyoko kwenye maeneo yasiyostahili. Ndani ya muda huo watu wote waondoe mifugo yao au wajitokeze kufuata taratibu zilizopo.

Ndugu Wananchi;
Nilisema nilipokuwa Mkoani Kagera na narudia tena leo kuwa baada ya siku 14 kupita, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendesha operesheni maalum ya kushughulikia matatizo hayo. Nilisema kuwa operesheni hiyo itafanyika katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja. Napenda kuwahakikishia kuwa hapatakuwa na mahali pa kukimbilia wala kujificha. Nawashauri wale wote wanaohusika na ujambazi, uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua muafaka sasa. Wasisubiri operesheni iwakute, wala wasifikirie kuwa hili ni jambo la kupita. Safari hii itakuwa endelevu.

Ndugu Zangu;
Hatuwezi kukubali hali hii niliyoikuta Mkoani Kagera ikaachwa kuendelea. Italeta madhara makubwa zaidi siku za usoni. Haiwezekani raia katika nchi yake, akose uhuru na usalama wa kutembea peke yake mpaka asindikizwe na Polisi. Na, baya zaidi hata Polisi nao wanashambuliwa na kuuawa watakavyo majambazi. Uhalifu huu lazima ukomeshwe, uishe na usijirudie tena.

Pia, haiwezekani hali ya watu kutoka nchi jirani kuingia nchini, kuishi na kufanya shughuli na kutoka watakavyo. Hatuzuii watu kuingia na kuishi Tanzania lakini wafuate sheria na taratibu za kuhamia na kuishi katika nchi yetu. Nchi yetu ina sifa na ukarimu huo. Hakuna uthibitisho mkubwa zaidi ya ule wa mwaka 1982, Rais Julius Nyerere wakati ule alipowaruhusu wakimbizi wanaopenda kuwa raia wa Tanzania wafanye hivyo. Wakimbizi 30,000 tu waliitumia fursa hiyo. Mwaka 2010 tuliwapa uraia wakimbizi 160,000 wa kutoka Burundi. Kwa sababu hiyo hatuoni sababu ya watu kufanya wanayoyafanya sasa kule Mkoani Kagera. Hatuwezi kuacha hali hiyo iendelee ilivyo.

Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa Mkoani Kagera nilielezea kusikitishwa kwangu na vitendo vya baadhi ya watendaji na viongozi wa vijiji na wananchi kuwaruhusu watu kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria. Nimewataka waache mtindo huo. Nimeagiza na wao wajumuishwe katika operesheni ijayo. Watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo haramu wachukuliwe hatua zipasazo kisheria. Aidha, niliwataka Maafisa wa Uhamiaji watimize ipasavyo wajibu wao. Ukweli ni kwamba, mambo haya kuendelea kwa muda mrefu kiasi hiki ni kwa sababu ya udhaifu wa mamlaka husika. Vile vile, nimewataka TAKUKURU nao watimize wajibu wao. Hapa kuna uthibitisho tosha wa kuwepo kwa vitendo vya rushwa vinavyohusisha wahamiaji hao na maofisa wa vijiji na idara husika za Serikali. Mimi naamini kama TAKUKURU ikiwabana na Uhamiaji wakichemka vya kutosha tatizo hili lingepungua sana au hata kutokuwepo kabisa.

Uhusiano na Nchi ya Rwanda

Ndugu wananchi;
Katika kipindi cha miezi miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi yetu na Rwanda unapitia katika wakati mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo. Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kama majirani kila mmoja anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.

Napenda kusisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yo yote jirani au yo yote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.

Ndugu Wananchi;
Ukweli ni kwamba wakati wote tumekuwa tunajihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi zetu. Hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu na nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha. Sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa aina yo yote. Busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo. Waingereza wanasema “two wrongs do not make a right”.

Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi. Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika Umoja wa Afrika na hata kimataifa. Uhusiano unaelekea kupata mtikisiko baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema cho chote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.

Kwa kweli nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely out of proportion and out of context. Mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda wetu. Tumekuwa tunakutana katika mikutano na vikao mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea. Wakati wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana ushauri ni wajibu wetu wote. Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo.

Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia kusema kuwa mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya na Rwanda. Tunapenda tuendelee kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi yetu ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu. Hatupendi kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.

Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza, naomba kutumia nafasi hii pia kuwatakia Waislamu wote nchini heri na baraka tele katika kukamilisha ibada muhimu ya kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Naomba tuendelee kuwatakia heri ili wamalize salama na tuweze kusherehekea kwa furaha na bashasha tele siku kuu ya Idd el Fitr pindi itakapowadia.

Mwisho kabisa, nawaomba Watanzania wenzangu wote tuendelee kushirikiana na kuishi kwa upendo, umoja na mshikamano kama ilivyo kawaida yetu.

Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni Sana Kwa Kunisikiliza.

Thursday, August 1, 2013

Mbunge wa CCM Mtwara afutiwa shitaka la uchochezi


Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara imemfutia shtaka la kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM)Hasnein Murji .

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo iliposomwa Julai 3, mwaka huu kwa madai ya kuwa hati ya mashtaka ni dhaifu kisheria na haionyeshi ni makosa yapi mtuhumiwa aliyotenda.

Wakili Kibatala alieleza mahakama kuwa kifungu cha 129 na 132 cha sheria ya mwenendo wa makosa jinai ni lazima mshtakiwa aelezwe mashtaka yake wazi wazi yanayomkabili.

Murji alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo akikabiliwa na kesi ya uchochezi anayodaiwa kuifanya Januari 19,mwaka huu katika eneo la Ligula mkoani hapa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Dynes Lyimo alifuta shtaka hilo na kumwachia mshtakiwa huru baada ya kesi hiyo kuahirishwa tangu Julai 3,mwaka huu.

Wakati huo huo viongozi wa upinzani Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF wanaokabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri wamefikishwa mahakamani.

Waziri Mkuu Mizengo Pendo ashtakiwa rasmi


Kituo cha Sheria na Utetezi wa Haki za Binadamu (LHRC) na Chama Cha Wanasheria Tanzanyika vimefungua kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, vikiomba mahakama hiyo itoe tafsiri za kisheria katika baadhi ya Ibara.

Kesi hiyo ya Kikatiba ambayo imepewa namba 24 ya mwaka huu, na ambayo bado haijapangiwa jaji, wadaiwa ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Taasisi hizo ambazo zinatetewa na mawakili wa kujitegemea Harold Sungusia, Francis Stolla na wengine 17, kwa mujibu wa hati yao ya madai, walalamikaji hao wamewasilisha jumla ya maombi mawili ambayo wanaomba mahakama itoe tafsiri ya kisheria katika Ibara hizo kwa kuwa wamewasilisha kesi hiyo ya Kikatiba chini ya sehemu ya Tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inaainisha Haki na Wajibu Muhimu.
     Wakili Sungusia alilitaja ombi la kwanza kuwa, wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa ibara ya 100(1) ya Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa majadiliano kwa wabunge wawapo ndani ya bunge ambayo inasomeka hivi: “kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katikaMahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.”

   Wakili Sungusia anadai kuwa Ibara hiyo ina ubaguzi ndani yake kwani inayoa uhuru kwa mbunge kujadili ndani ya bunge na wakati anajadili jambo hata kama amevunja haki za mtu mwingine hataweza kushitakiwa wala kuhojiwa jambo ambalo anadai linakinzana na Ibara ya 13(2) ya Katiba ambapo Ibara hii inasomeka hivi; “ Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake’.
‘...sisi tunaomba mahakama itamke wazi kuwa Ibara ya 100(1) inakwenda kinyume na matakwa ya Ibara 13(2). Zinakinzana, kwa kuwa ibara ya 100(1) ya Katiba inatoa haki tu kwa upande wa mmoja wa wabunge uhuru wao kutohojiwa na inawanyima haki ya kuwahoji au kuwashitakiwa wabunge wanaotoa kauli zao bungeni hata kama kauli hizo za wabunge zimevunja haki za wananchi,”alidai wakili Sungusia.

      Wakili Sungusia alilitaja dai la pili kuwa ni kuiomba mahakama hiyo itamke kuwa kauli ya Waziri Mku, Pinda ambayo ililitaka Jeshi la Polisi kuwapiga wale wote wanaokiuka amri za jeshi hilo, kama kauli hiyo nayo inalindwa na kinga iliyowekwa katika Ibara ya Ibara ya 100(2) ya Katiba ya nchi ambayo inasomeka hivi: ‘Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo.’

Katiba mkutano wa bunge uliomalizika hivi karibuni , Waziri Mkuu Pinda akiwa ndani ya bunge aliliagiza jeshi la polisi kuwapiga wale wote wanaokaidi amri za jeshi hilo, kwasababu serikali imeshachoshwa na vitendo vya baadhi ya wananchi wanaokaidi kwa makusudi amri za jeshi la polisi , kauli iliyoleta mhemko kwa jamii huku wengine wakiipinga utekelezaji wa agizo hilo na wengine wakiunga mkono, hali iliyosababisha LHRC hivi karibuni ilizungumza na waandishi wa habari wakimtaka Pinda afute kauli yake hiyo ama sivyo watamfikisha mahakamani.

Rejea ya habari: Happiness Katabazi, gazeto la TanzaniaDaima la Ijumaa, Agosti 2 mwaka 2013.

Wakati Sheikh Ponda akitangaza kugombea URAIS Polisi yatangaza kumkamata kwa kufanya mihadhara ya uchochezi


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar kimemtuhumu Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, kuwa anaendesha kampeni za uchochezi wa kidini.

Uchochezi huo umedaiwa kuhatarisha amani ya nchi, hivyo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kumchukulia hatua za kisheria.

Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu (NEC) Zanzibar, Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, alisema jana kuwa ni wiki moja sasa tangu Ponda afanye mihadhara kwenye misikiti ya Mbuyuni, Kwarara na Nungwi kisiwani Unguja.

Waride alisema kuwa hotuba za Sheikh Ponda alizozitoa kwa nyakati tofauti kwenye misikiti hiyo zinapandikiza mbegu ya chuki, kuondosha upendo na kuhatarisha amani.

Alisema matamshi yake ni hatarishi kwa amani na utulivu uliopo, kwani anawataka Waislamu kupigana vita ya dini (Jihad) na kushiriki harakati za kuikomboa Zanzibar, kwa madai kuwa serikali iliyoko madarakani inawakandamiza na kuwanyanyasa wananchi.

“Sheikh Ponda ni hatari, anapanda shari na chuki miongoni mwa wananchi, anahamasisha wananchi wafanye uasi, kulipiza visiasi na kutaka waingie barabarani kwa maanadano ya kutetea haki kama inavyotokea Misri,” alisema.

Aidha, alisema CCM imeshangazwa na ukimya wa vyombo vya ulinzi na usalama wa raia kumtazama kiongozi huyo bila ya kumchukulia hatua za kisheria wakati akiwatukana matusi ya nguoni viongozi wa serikali na chama tawala.

Aliongeza kuwa Sheikh Ponda huenda anatumiwa na mtandao wa vurugu ili kuharibu na kuvuruga amani ambapo hamu yake ni kuona damu ya wananchi ikimwagika na nchi ikiingia kwenye machafuko.

Kwa mujibu wa Waride, kitendo cha Ponda kulitumia jukwaa la dini na kufanya siasa misikitini hakikubaliki na kwamba kikiachiwa kiendelee kinaweza kuleta madhara na mgawanyiko.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema jeshi hilo limeanza kumtafuta Sheikh Ponda tangu walipopokea taarifa za kuendesha mihadhara ya uchochezi katika baadhi ya misikiti, ikiwa na lengo la kuibua chuki.

Mussa alisema kitendo anachokifanya kinakwenda kinyume cha sheria, hivyo kumtaka popote alipo ajisalimishe kwa hiari yake.

Tangu kuingia visiwani Zanzibar, Sheikh Ponda amekuwa akifungamana na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho wakipinga kitendo cha viongozi wa jumuiya hiyo kuendelea kubakia mahabusu baada ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa taifa.

Viongozi hao wa Uamsho wako mahabusu baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, kuwasilisha ombi la kufunga dhamana yao kwa kutumia sheria ya Usalama wa Taifa na marekebisho yake ya mwaka 2002

Tanzania daima.